Katibu Mkuu UVCCM Kenani Kihongosi atoa maelekezo kwa vijana nchini

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kenani Kihongosi amewataka vijana kutumia mitandao ya kijami kwa kupata kipato na kupashana habari zenye tija na si kudhalilisha utu wa viongozi wa chama na Taifa.
Ameyasema hayo leo Juni 25,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na vijana wa umoja huo kwenye hafla fupi ya kukaribishwa kwake Makao Makuu mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.

Kihongosi amesema, vijana wengi hapa nchini wamekuwa wakijihusisha vibaya na mitandao ya kijamii kwa viongozi,kudhalilishana, kudhihaki jambo ambalo ni kinyume na ukiukwaji wa sheria za chama na Taifa.

"Katika mitandao kuna mijadala isiyo na tija kila mmoja atumie mitandao vizuri,   tutumie mitandao kwa kupata kipato ndugu zangu na kupashana habari na si vinginevyo na niwasihi chama hakitasita kuwachukulia hatua kali wale watakaokwenda kinyume na maadili.

"Badala ya kushinda kwenye mitandao bila tija niwasihi kutumia mitandao hiyo kutangaza miradi ya Serikali inayotekelezwa kwenye eneo unaloishi huku ukitafuta fursa za ajira jambo ambalo litawafanya kuchochea maendeleo kwa jamii,"amesema Kihongosi.

Aidha, ameutaka umoja huo kuepuka migogoro katika kazi hususani majungu,dharau na ugomvi ambayo yamekuwa kero kubwa bali wadumishe umoja , upendo na mshikamano viwe nguzo ili kulitumikia Taifa.

Katika hatua nyingine amewakemea vikali baadhi ya vijana ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwabeba na kuanza kuwanadi wagombea kabla ya muda wake jambo ambalo sio sahihi na utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kudai wasubiri mwakani ili waanze kampeni.

Vilevile amewataka viongozi wa umoja huo kutembelea sehemu zenye changamoto za vijana kama wafanyakazi wa hotelini,madereva bajaji,bodaboda, na mama ntilie ,machinga ,mafundi ujenzi, umeme, wakulima, wavuvi, pamoja na makundi yote ili kujua changamoto wanazokumbana nazo na kuzifikisha kwenye chama ili zipatiwe ufumbuzi kwa maslahi ya Serikali.

"Niwatake viongozi huko mikoani na wilaya zote kufika kwenye halmashauri za wilaya muongee na wakurugenzi namna ya kupewa zile asilimia zinazotengwa kuwakopesha vijana bila riba ili waweze kufanya biashara mbalimbali na kujikwamua kiuchumi kwani fedha hizo zimekuwa zikitumika kwa watu wengine,"amesema Kihongosi.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri Ofsi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye Ulemavu ,Ummy Nderiananga amewataka vijana kuiga mfano wa Katibu Mkuu huyo kuwa na nidhamu ,kujituma katika chama ili kupata nyadhifa mbalimbali.

Amesema, Ofsi ya Waziri Mkuu kuna miradi mingi ambayo inahusu vijana hivyo ni fursa kufika kwake kuweza kuona ni namna gani atawasaidia huku akisema tayari kuna nafasi milioni nane za ajira ambazo zimetengwa kwa ajili ya Vijana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news