TAARIFA KWA UMMA
Chama Cha ACT Wazalendo kimeipokea kwa masikito makubwa kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na Katiba Mpya visubiri kwanza yeye asimamishe nchi na kujenga uchumi wa Taifa.
Kauli hiyo aliyoitoa jana kwenye kikao chake na Wahariri wa Vyombo Vya Habari kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam kuadhimisha Siku 100 za Utawala wake ni mwiba uliowachoma wapenda demokrasia, watetezi wa haki za binadamu na Watanzania kwa ujumla.
Kuhusu Katiba Mpya, ACT Wazalendo tunaamini kuwa Katiba ni msingi na kichocheo cha Maendeleo.
Hakuna maendeleo ya uhakika yanayoweza kupatikana bila kwanza kuweka msingi madhubuti wa Kikatiba.
CCM ambayo imekuwepo madarakani tangu uhuru haiwezi kuwakosesha wananchi haki yao ya kupata Katiba Mpya kwa kisingizio cha kujenga uchumi wa nchi.
Kuhusu mikutano ya hadhara, hii ni haki inayolindwa na Katiba na Sheria. Katiba ya Tanzania (Ibara ya 3) na Sheria ya Vyama vya Siasa (Kifungu cha 11) vinatoa haki ya Vyama vya Siasa kukusanyika.
Rais wa Nchi ambaye ameapa kuilinda na kuitetea Katiba na Sheria za Nchi hapaswi kuzuia haki ambayo imetolewa na kulindwa na Sheria.
WITO WETU:
Tunatoa wito kwa Rais Samia Suluhu atafakari upya msimamo wake kuhusu Katiba Mpya na haki ya Vyama vya Siasa kufanya mikutano ya hadhara.
Iwapo ataendelea na msimamo huo, bila shaka, atakuwa ameutia doa kubwa utawala wake na kupanda mbegu itakayolirudisha nyuma na kuligawa Taifa.
Imetolewa na Janeth Rithe, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, ACT Wazalendo. 29 Juni 2021.
Tags
Habari