Lengai Ole Sabaya, wenzake tutawaona tena Julai 2 hapa Sekei

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Lengai Ole Sabaya ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na wenzake wawili wamesomewa mashtaka mawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliyopo Sekei.

Sabaya akiwa na Sylivester Nyingu (26) maarufu Kicheche na Daniel Mbura (38) wamesomewa mashtaka hayo yanayowakabili kati ya mashtaka sita waliyonayo wakiwemo wenzao watatu.

Mashtaka mengine manne yanayowakabili watuhumiwa hao ni ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi, kuomba rushwa na kuunda genge la uhalifu huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria.

Watuhumiwa hao ambao walikana mashtaka yanayowakabili wanatetea na wakili, Moses Mahuna jijini hapa.

Hayo yamejiri leo Juni 18,2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mkoani Arusha huku mashtaka mengine manne upelelezi wake ukiwa bado haujakamilika.

Tumaini Kweka ambaye ni Wakili Mkuu wa Serikali amemweleza Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salome Mshasha kuwa, upande wa mashtaka umekamilisha upelelezi na upo tayari kuwasomea maelezo watuhumiwa.

Aidha,Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Tarsila Gervas amesema Februari 9, 2021 katika Mtaa wa Bondeni, Lengai Ole Sabaya akiwa na watuhumiwa wenzake wawili walitenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Ilidaiwa ni baada ya kuvamia duka la Said Saad na kuwaweka chini ya ulinzi jiini Arusha.

Amedai,Lengai Ole Sabaya na walinzi wake, Sylivester Nyingu (26) maarufu Kicheche na Daniel Mbura(38) walitenda kosa hilo baada kumfunga pingu na kumpiga Bakari Msangi ambaye ni Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Sombetini na kumuibia 390,000.

Ilidaiwa katika tukio hilo wakitumia silaha, Lengai Ole Sabaya na walinzi hao pia walimpiga kwa mateke, kumtishia silaha na kumpora simu na Shilingi 35,000, Ramadhani Ayoub.

Aidha, kutokana na makosa hayo kutokuwa na dhamana watuhumiwa walirudishwa mahabusu gereza kuu la Kisongo baada ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Julai 2, mwaka huu.
Jun 4,2021 Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani hapa kwa mara ya kwanza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news