MIPANGO MIKAKATI KWA VYOMBO VYA HABARI SERIKALI AWAMU YA SITA YAWEKWA WAZI
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO,Ndg. Gerson Msigwa akitoa taarifa ya Mipango na Mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa vyombo vya habari leo Juni 5, 2021 Jijini Dodoma.
YALIYOJIRI LEO JUNI 5, 2021 DODOMA, WAKATI MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, GERSON MSIGWA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MASUALA MBALIMBALI YA SERIKALI
#Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwangu na kuniteua kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali.
#Nawashukuru waandishi wa habari, wahariri na wadau wa wote wa habari ambao wameendelea kutekeleza jukumu la kutoa taarifa mbalimbali ambazo waandishi wa habari mmekuwa mkizihitaji.
#Leo ni siku 80 tangu tuondokewe na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Na ni siku 78 tangu Mhe. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya 6.
#Tunamshukuru Mungu kwa nchi yetu kuheshimu Katiba na utawala wa Sheria, baada ya kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Serikali, mchakato wa aliyekuwa Makamu wa Rais ulifanyika na kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa amani na utulivu mkubwa na sasa tunaye Mhe. Samia Suluhu Hassan (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).
Hali ya Serikali
#Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuongoza nchi, kusimamia ulinzi na usalama, kusimamia rasilimali za Taifa.
#Kwa niaba ya Serikali napenda kuwashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kuwa na imani na Serikali yao, kushirikiana nayo na kutekeleza masuala mbalimbali ambayo wanapatiwa kama mwongozo kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na mipango mbalimbali.
#Uzalishaji mali unaendelea, pamoja na kwamba dunia inatikiswa na janga la virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Korona (Uviko-19) na uzalishaji wa maeneo mengi umetikiswa kwa kiasi kikubwa.
#Serikali inaendelea kuwahimiza Watanzania wote kuendelea kuchapa kazi za uzalishaji mali kwa juhudi na maarifa huku wakichukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Korona, zikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka.
Hali ya Uchumi
#Hali ya Uchumi wetu ni nzuri japo na sisi tumepatwa na madhara ya Korona kama ilivyo kwa nchi zingine dunia. Uchumi wetu uliokuwa unakua kwa wastani wa asilimia 6.9 umeshuka kidogo hadi wastani wa asilimia 4.7, na matarajio ni kuwa uchumi wetu utaendelea kukua vizuri kutokana na hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa.
#Mfumuko wa bei kwa sasa ni wastani wa asilimia 3.3% ambayo ni kiasi kizuri. Akiba ya fedha za kigeni ni nzuri ambazo zinatosha kununua bidhaa na huduma kwa muda wa zaidi ya miezi 4.7.
Maendeleo ya Miradi ya Kimkakati
#Mhe. Rais ambaye ni Mkuu wa Serikali ameshatoa msimamo wake wa uongozi kwamba ataendeleza mazuri yote yaliyofanywa na watangulizi wake yaani Marais Wastaafu na waliotangulia mbele za haki na ataanzisha miradi mipya.
#Reli ya kisasa/Standard Gauge Railway (Dar es Salaam – Morogoro (km 300) 91%, Morogoro – Makutupora (km 422) 61% na ujenzi wa reli Mwanza – Isaka umeanza ambapo Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 372.34 za ujenzi wa kilometa 341 za reli hiyo.
#Bwawa la Julius Nyerere katika mto Rufiji ujenzi wa mradi umefikia 52% kutoka asilimia 45.
#Ununuzi wa ndege ambapo ndege 8 zipo, na ndege 3 zitafika wakati wowote kuanzia sasa.
#Ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi mkoani Mwanza umefikia 27% ikiwa ni mradi utakaogharimu shilingi Bilioni 712 hadi kukamilika kwake Februari 2024.
#Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam daraja la Tanzanite 77.19%, Flyover za Chang’ombe na Kurasini, BRT 2 (barabara ya Kilwa), DMDP, upanuzi wa barabara ya Morogoro, huku kote kazi zinaendelea.
#Ujenzi wa meli Mv- Mwanza (Hapa Kazi Tu) umefikia 74%. Na katika mwaka wa huu kuna mikataba 9 ambapo ujenzi wa meli mpya 3 zitajengwa katika maziwa makuu, meli mpya 1 katika Bahari ya Hindi. Pia kutakuwa na ukarabati wa meli 5 katika maziwa ya Victoria na Tanganyika.
Huduma za kijamii zimeendelea kutolewa kama kawaida
#Afya, kati ya Machi na Juni, 2021, Kibali cha ajira kwa watumishi wa umma 4,127 kimetolewa kwa Wizara ya Afya.
#Serikali imetoa shilingi Bilioni 121.3 kwa ajili ya ununuzi wa dawa zinazokwenda katika mikoa mbalimbali na Shilingi Bilioni 43.5 zimetolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa Hospitali za kanda, za rufaa za mikoa.
#MOI imeanza kutoa matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa ubongo bila kufungua kichwa pamoja na kupandikiza figo, kuzibua mishipa ya moyo kwa tundu dogo, upasuaji wa nyonga, magoti, kibiongo na mfumo wa fahamu.
#Vifaa tiba vimeendelea kupelekwa katika hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Sekou Toure Mwanza vifaa vilivyopelekwa ni CT Scan, Ultra Sound sawa na Shilingi Bilioni 2.228; Bugando imepelekwa MRI ya Shilingi Bilioni 2.43; Mwananyamala CT Scan ya Shilingi Bilioni 1.444 na vifaa vingine vimesambazwa katika hospitali za rufaa za mikoa na hospitali za wilaya.
Kuhusu Ugonjwa wa Korona (Uviko-19)
#Mheshimiwa Rais ameamua kuimarisha juhudi za kupambana na janga la Korona kwa kutoa nafasi kwanza kwa Wataalamu wetu wakiongozwa na Prof. Said Aboud kufanya tathmini ya kitaalamu na kuishauri Serikali juu ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huu.
#Mheshimiwa Rais amekabidhiwa mapendekezo hayo yenye mpango kazi wa kutafuta rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Taifa wa kukabiliana na janga la ugonjwa wa Korona (Uviko-19).
#Mapendekezo ya mpango kazi wa uratibu wa utoaji wa chanjo ya ugonjwa huo yaliyowasilishwa na kamati ya wataalamu aliyoiunda kwa ajili ya kuishauri Serikali juu ya kukabiliana na ugonjwa huo.
#Balozi na taasisi mbalimbali za Kimataifa hizi zimeruhusiwa kuleta chanjo kwa ajili ya raia wa nchi zao na watumishi wao.
Ukusanyaji wa Mapato
#Ukusanyaji wa kodi unakwenda vizuri, na Serikali inawapongeza Watanzania wote kwa kuitikia wito wa kulipa kodi. Kodi ni maendeleo.
#Mwenendo wa Makusanyo ya Kodi kuanzia Januari 2021 hadi Machi 2021. Mwezi Jan 2021: malengo yalikuwa Tril. 1.68, makusanyo Tril. 1.34 sawa na asilimia 79.8; mwezi Feb 2021: malengo yalikuwa Tril. 1.61, makusanyo Tril. 1.33 sawa na asilimia 82.9; mwezi Machi 2021: malengo yalikuwa Tril. 1.99 makusanyo Tril. 1.67 sawa na asilimia 84.1; mwezi April 2021 malengo yalikuwa Tril. 1.61 makusanyo Tril. 1.34 sawa na asilimia 83.2 na mwezi Mei 2021: Malengo 1.619 makusanyo yalikuwa 1.33 sawa na asilimia 82.
#Serikali inakusanya kodi kama kawaida kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo kugharamia mishahara, kuhudumia deni la Taifa, kugharamia miradi ya maendeleo.
Katika Masuala ya Diplomasia
#Nchi yetu imeendelea kutekeleza vizuri diplomasia yake ya uchumi. Tumeona jinsi Mhe. Rais anavyochukua hatua madhubuti za kuimarisha uhusiano wetu na nchi mbalimbali dunia. Na dhamira ni kuwa Tanzania isiende pekee yake lazima kwenda na wenzetu.
#Ziara 2 alizofanya nchini Uganda na ziara rasmi ya Rais wa Uganda hapa Tanzania matokeo yake ni kukamilika kwa mchakato wa kimikataba wa utekelezaji wa mradi Dola Bilioni 4.16 wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga Tanzania lenya urefu wa kilometa 1,443 ambapo kati yake kilometa 1,147 zinapita Tanzania katika mikoa 8 na Wilaya 24.
#Manufaa ya mradi huu kwa nchi yetu ambayo licha ya kumiliki asilimia 15 ya hisa zote za kampuni, kutakuwa na ajira takribani 10,000 zitazalishwa, kutakuwa na mrabaha wa asilimia 60, na kutakuwa na kodi nyingi ambazo tutazipata. Mradi huu sasa upo tayari kuanza ujenzi na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 36.
#Ziara rasmi ya Kenya, imeimarisha zaidi uhusiano wetu na Kenya. Hivi sasa wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya wanafanya biashara zao bila vikwazo na kupitia jukwaa la wafanyabiashara lililofanyika Jijini Nairobi.
#Mchakato wa kujenga soko la pamoja mpakani ili wafanyabiashara wa Tanzania wasilazimike kuzifuata bidhaa ndani ya Kenya bali watazipata katika soko la pamoja linalojengwa na wafanyabiashara wa Kenya hawatalazimika tena kuingia vijijini kutafuta mazao watapelekewa sokoni mpakani.
#Mhe. Rais ameshiriki mkutano kwa njia ya mtandao ulioitishwa na Rais wa Ufaransa Mhe. Emmanuel Macron kujadili juu ya athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la Korona Barani Afrika na namna nchi zilizoendelea na mashirika ya kimataifa yanaweza kusaidia kuokoa uchumi wa nchi za Afrika.
#IMF imepanga kutumia Dola za Marekani Bilioni 650 katika awamu ya pili ya mpango wa kusaidia kwa dharura uchumi wa nchi mbalimbali zinazoendelea kutokana na madhara ya janga la korona, ambapo Mhe. Rais ameagiza Wizara ya Fedha kuandaa maandiko ili nchi yetu inufaike na mpango huu.
#Mhe. Rais ameshiriki mazungumzo na mtandao wa viongozi wanawake wa Afrika. Mtandao huu unaongozwa na Rais Mstaafu wa Liberia Mhe. Ellen Sirleaf, pamoja na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Antonio Gutterres.
Uhuru wa Vyombo vya Habari
#Mhe. Rais aliagiza kufunguliwa kwa Televisheni Mtandao na hakuagiza kufunguliwa kwa vyombo vyote kama ambavyo baadhi yetu tulikuwa tunapotosha juu ya kauli ya Mhe. Rais.
#Rais alisisitiza kwamba vyombo vya habari vifanye kazi kwa uhuru na kuzingatia sheria na taratibu. Sheria ya huduma za Habari ya mwaka 2016 ipo na inaendelea kufanya kazi.
#Vyombo vya habari ambavyo vimefungiwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameshatoa maelekezo kuwa wamiliki wa vyombo hivyo wawasilishe hoja zao ili zisikilizwe na kufanyiwa na utekelezaji wa agizo hili unaendelea kufanyika na baadaye Serikali itaamua.
Sekta Binafsi
#Serikali inawapongeza na kuwatia moyo wafanyabiashara na wawekezaji wote waliojitokeza kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini kwetu. Sekta Binafsi ni injini ya uchumi wetu, inazalishaji ajira, inaleta kipato kwa Serikali na inaimarisha ustawi wa wananchi.
#Mhe. Rais Samia amekuwa kinara kwenye eneo hili na tayari ametoa maelekezo kadhaa ya kuhakikisha sekta binafsi inaimarika kwa kuondoa vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi, unyanyasaji dhidi ya wafanyabiasha na kujenga miundombinu inayohitajika.
#Mhe. Rais amekutana na viongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) amepokea mawazo yao na ameahidi kuyafanyia kazi. Pia wakati wowote kutafanyika mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara (TNBC) ambao yeye Mhe. Rais ni Mwenyekiti na matarajio ni kuwa masuala muhimu ya kuboresha biashara na uwekezaji yatajadiliwa.
#Serikali sasa imeamua kuwatelekeza wafanyabiashara wadogo (Machinga, Mama Lishe n.k) wote mmeona juzi tu Mhe. Rais alikuwa Soko la Kariakoo ambako amejionea mazingira ya wafanyabiashara wadogo na ameahidi kufanyia kazi changamoto zinazowakabili.
Bandari ya Dar es Salaam
#Upanuzi unaendelea katika gati namba 1 hadi 7 ambapo gati namba 1 hadi 5 ujenzi wake umekamilika na zinafanyakazi na ujenzi unaendelea katika gati namba 6&7 unaotarajiwa kukamilika mwezi wa 8, 2021.
#Ufanyaji kazi wa Bandari unaongezeka ambapo idadi ya meli zinaongezeka na mapato yanakua, mwezi Aprili mapato yalikuwa Shilingi Bilioni 73.2, Mei Shilingi Bilioni 84.6 na hiki ni kiwango kikubwa ikilinganishwa na mapato ya mwezi Machi ambapo yalikuwa shilingi Bilioni 80.2.
Utalii
#Nchi yetu imechukua hatua madhubuti za kuulinda utalii kwa kuzingatia miongozo na masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) dhidi ya ugonjwa wa Korona kwa kuwahakikishia watalii usalama wao wakiwa hapa Tanzania katika vivutio vyetu vya utalii.
#Matarajio yetu ni kuwa watalii watazidi kuongezeka na mmeona watu maarufu duniani wanakuja
Imeandaliwa na Idara ya Habari- MAELEZO
Tags
Habari