Bismillah It Rahmaanir Rahiim
SHURA YA MAIMAMU TANZANIA
SHEIKH MSELEM SHEIKH FARID WAKO NYUMBANI ZANZIBAR
Masheikh zetu wawili wako majumbani kwao na familia. Tutaendelea kukupeni taarifa awamu kwa awamu.
Lengo ni kutoa taarifa za kweli na zilizozingatia mambo yote muhimu.
Aidha viongozi wa Shura Taifa wako angani wakielekea Zanzibar.
Ibrahimu Zuberi Mkondo
Msemaji wa Shura ya Maimamu Tanzania
0713118812
Viongozi wawili kati ya 36 wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed na Mselem Ali Mselem waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi wameachiwa huru.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu ameieleza Mwananchi Digital leo Jumatano Juni 16, 2021 kuwa amewafutia mashtaka viongozi wote wa jumuiya hiyo na kilichobaki sasa ni taratibu za kutoka gerezani.
Wawili hao ambao walikuwa mahabusu tangu mwaka 2014 pamoja na wenzao kutokana na kukabiliwa na mashtaka hayo ambayo hayana dhamana wameachiwa huru jana Jumanne Juni 15, 2021 baada ya DPP kuwafutia mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Taarifa za kuachiwa huru kwa viongozi hao zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia jana jioni zikieleza kuwa viongozi hao wawili ndio wameachiwa huru na mmoja wa mawakili wao, Juma Nassoro amelieleza Mwananchi Digital kuwa wameshapelekwa majumbani mwao.
Katika ufafanuzi wake Mwakitalu amesema, “ni kweli wameachiwa huru. Nimewafutia wote mashtaka yaliyokuwa yanawakabili. Sasa suala la kutoka gerezani kama wameshatoka wote au wangapi hilo ni suala la taratibu za Magereza lakini mimi nimewafutia mashtaka wote.”
Washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kujihusisha na makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha sheria ya kuzuia ugaidi ya 2002 Januari 2013 na Juni 2014.
Awali walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam kwa hatua za awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa usikilizwaji kamili wakikabiliwa na jumla ya mashtaka 25.
Lakini Aprili 23, 2021 Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka 14 baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wao, Daimu Halfani, Juma Nassoro, Jeremiah Mtobesya na Abubakar Salum kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka hayo kwa kuwa makosa wanayotuhumiwa yanadaiwa kutendeka Zanzibar.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake huo uliotolewa na Jaji Mustapha Ismail baada ya kusikiliza hoja za pande zote, hoja za pingamizi la utetezi na majibu ya upande wa mashtaka ulioongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga akisaidiwa na wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Paul Kadushi, ilikubaliana na hoja za utetezi.
Jaji Ismail alisema pamoja na mambo mengine kuwa kwa makosa ambayo yanadaiwa kutendeka Zanzibar, jukwaa sahihi la kuwashtaki washtakiwa ni katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Jaji Ismail aliuamuru upande wa mashaka kufafanua marekebisho katika hati ya mashtaka kwa kuyaondoa mashtaka hayo na kubakiza yale ambayo yamedaiwa kutendeka katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tanzania Bara ambayo ndio mahakama hiyo ina uwezo wa kuyasikiliza.(JF).
Tags
Habari