NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua hukumu ya kesi ya uchochezi dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake na kuamuru warejeshewe kiasi cha shilingi milioni 350 walicholipa kama faini.
Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Irvin Mgeta ambapo Freeman Mbowe na wenzake walihukumiwa katika Mahakama ya Kisutu Machi 10, 2020 kulipa faini ya shilingi milioni 350.
Mheshimiwa Mbowe na wenzake walihukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwenye makosa 12 ikiwemo la kufanya maandamano.
Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo walikuwa ni Esther Matiko, Mchungaji Peter Msigwa, Salum Mwalimu, John Mnyika, Halima Mdee, John Heche, Ester Bulaya na Dkt. Vicent Mashinji.
Hukumu hiyo iliyochukua saa 4, kuanzia saa 7 mchana hadi saa 11 jioni, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi 23 baina ya utetezi na Serikali.
Awali alipokuwa akisoma mashitaka hayo Februari 22, 2018, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka 2018 maeneo ya Viwanja vya Buibui na Barabara ya Kawawa, Mkwajuni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika shitaka la kwanza la kula njama, kwa pamoja inadaiwa Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam, walikula njama pamoja na wenzao ambao hawakuwa mahakamani, ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali, mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko kutawanyika.
Pia ilidaiwa kuwa Februari 16,2018 katika Viwanja vya Buibui na Mwananyamala Kinondoni, washtakiwa hao wakiwa wamekusanyika na azma ya pamoja waliitekeleza, walifanya mkusanyiko usio halali na kusababisha watu waogope na kusababisha uvunjïfu wa amani.
Shitaka lingine washitakiwa hao walidaiwa kuwa Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui Mwananyamala na Barabara ya Kawawa Kinondoni, kwa pamoja na wenzao 12 ambao hawakuwepo mahakamani, walitekeleza mkusanyiko ama maandamano yasiyo halali wakiwa na lengo la kuvamia ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kuĺeta hofu ya uvunjifu wa amani.
Nchimbi alidai kuwa Februari 16,2018 katika Barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni, washtakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawakuwa mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Ofisa wa Polisi, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani, ambao ulisababisha hofu na hatimaye kifo cha Akwilina na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.
Shitaka lingine lilimkabili Mbowe ambalo ni la kuhamasisha chuki inadaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Mbowe wakati akihutubia wananchi wa jimbo hilo, alihamasisha chuki isivyo halali kwa kutoa matamshi.
Pia Mbowe alidaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika mkutano wa umma uliofanyika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Mbowe alitamka maneno ya uchochezi.
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa ya kuinua hali ya kutoridhika miongoni mwa watanzania dhidi ya serikali halali iliyopo.
Naye Halima Mdee alidaiwa kuwa Februari 16,2018 akiwahutubia wakazi wa Kinondoni alitamka maneno ya uchochezi.
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na lengo kuhamasisha hisia za chuki miongoni mwa watanzania.
Shitaka lingine ni kuhamasisha hali ya kutoridhika, Heche anadaiwa kuwa Februari 16,2018 katika Viwanja vya Buibui alitamka maneno ya uchochezi.
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na lengo kuhamsha hali ya kutoridhika miongoni mwa watanzania dhidi ya utawala uĺiopo madarakani.
Shitaka lingine lilikuwa la uchochezi wa uasi, lililomkabili Mbowe, alidaiwa kuwa Februari 16,2018 katika maeneo hayo, alihutubia mkutano wa hadhara na kutamka
maneno ya uchochezi.
Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na nia ya kuleta chuki na hali ya manung’uniko miongoni mwa jamii dhidi ya utawala uliopo madarakani.
Shitaka la uchochezi wa uasi, lilimkabili tena Mbowe akidaiwa kuwa Februari 16,2018 katika maeneo hayo mkoani Dar es Salaam, Mbowe alitoa matamshi ya kupandikiza chuki na dharau kwa upande wa raia wa Tanzania dhidi ya mamlaka halali.
Mashitaka mengine yalikuwa ni kushawishi utendaji wa kosa la jinai, lililomkabili mshtakiwa wa pili Mchungaji Peter Msigwa, katika maeneo hayo hayo, Msigwa alidaiwa kushawishi raia na wakazi wa eneo hilo, kutenda kosa la jinai, kwa kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.
Pia mashtaka mengine ambayo yalimkabili mshtakiwa, Ester Bulaya alidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huo katika Viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar es Salaam alïtenda kosa la kukaidi amri halaĺi ya tamko.