Na James K. Mwanamyoto,Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi, ujulikananao kama SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) aliouzindua leo jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kushoto kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.
Akizindua mfumo huo leo ofisini kwake jijini Dodoma, Mhe Mchengerwa amesema, uzinduzi wa mfumo huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma na wananchi.
Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo huo utamuwezesha yeye na wasaidizi wake kupata taarifa za malalamiko yanayohusu huduma zinazotolewa katika taasisi za umma, ikiwa ni pamoja na kupokea maoni, pongezi kwa Mhe. Rais na Ofisi yake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijiandaa kubonyeza kitufe leo jijini Dodoma ili kuzindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU). Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi.
Amefafanua kuwa, mfumo huo pia utawawezesha kufanya ufuatiliaji wa namna malalamiko yanavyopokelewa na kufanyiwa kazi na kuongeza kuwa, mfumo unampa nafasi ya kutoa maelekezo ya ushughulikiwaji wa malalamiko hayo pale anapoona kuna ulazima wa kufanya hivyo.
“Popote nitakapokuwa, iwe safarini, ofisini au nyumbani, nitaweza kuona malalamiko yote yanayowasilishwa ofisini kwangu na namna yanavyofanyiwa kazi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amesema mfumo huo ni rafiki kwa watumiaji, hivyo kila mtumishi na mwananchi mwenye hoja ataweza kuutumia bila changamoto yoyote kwa njia ya tovuti kwa anuani ya www.swu.utumishi.go.tz, simu janja kwa kupakua SWU kutoka kwenye play store, na simu ya kawaida kwa kutumia msimbo wa *152*00# na kuchagua namba 9 na baadae namba 2 ili kuwasilisha malalamiko.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na vyombo vya habari kabla ya kuzindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) leo jijini Dodoma.
Aidha, katika kuadhimisha siku 100 za utendaji kazi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Mhe. Mchengerwa amezindua Jarida la Utumishi la Habari na Matukio ili kuuhabarisha umma namna Ofisi yake inavyomsaidia Mhe. Rais kutekeleza jukumu la usimamizi wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, jarida hilo litauhabarisha umma juu ya mafanikio ya Serikali yanayopatikani na utekezaji wa majukumu kwenye eneo la Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
“Jarida hili litakuwa linatoka kila baada ya miezi mitatu na litakuwa na maudhui ya utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa na matukio mbalimbali ambayo ofisi imekuwa ikiyafanya kwa masilahi ya umma hapa nchini,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi kabla ya uzinduzi wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) leo jijini Dodoma.
Mhe. Mchengewa ametoa wito kwa watumishi wenye habari za kiutumishi na utawala bora zenye manufaa kwenye utumishi wa umma na umma kwa ujumla kuwasilisha taarifa hizo ili ziweze kuchapishwa kwenye jarida hilo.
Awali akimkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzindua mfumo huo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, amefarijika kuona utekelezaji wa maelekezo ya kuanzishwa kwa mfumo wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi na wananchi umekamilika.
Mhe. Ndejembi amesema, anakumbuka siku ya kwanza ya Mhe. Mchengerwa kuripoti kazini, alitoa maelekezo ya kufanya kazi kidigitali katika kusikiliza kero, kupokea malalamiko na maoni ambayo yatatumika kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, hivyo amefurahi kuona mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI kuzinduliwa rasmi.
Mwonekano wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) uliozinduliwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Waandishi wa Habari kwenye uzinduzi wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) leo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akionyesha jarida la Utumishi Habari na Matukio mara baada ya kuzindua jarida hilo leo jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi akishiriki uzinduzi wa jarida hilo na kushoto kwake ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.
Akitoa neno la utangulizi kabla ya uzinduzi, Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro amempongeza Mhe. Mchengewa kwa kuwahamasisha watendaji wake kutekeleza majukumu kwa njia ya kidijitali ili kurahisiha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma na wananchi.
“Mfumo huu wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI ni zao la hamasa yako ya utatuzi wa changamoto za watumishi na wananchi zitakazowasilishwa kupitia mfumo huo”, Dkt. Ndumbaro ameeleza.
Mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI uliobuniwa na wataalam wa ndani wa TEHAMA umelenga kupunguza au kuondoa kabisa kero na malalamiko ya Watumishi wa Umma na wananchi kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani ameazimia katika utawala wake.
Tags
Habari