Mkandarasi Barabara ya Mwigumbi-Maswa atii agizo la Kafulila

Na Derick Milton, Simiyu

Siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila kuzuia malipo kwa mkandarasi CHICCO anayejenga Barabara ya Mwigumbi mkoani Shinyanga hadi Maswa mkoani Simiyu kutokana na kujenga chini ya kiwango mradi huo na kuagiza arudie, mkandarasi huyo ameanza utekelezaji wa agizo hilo.
DIRAMAKINI Blog imeshuhudia Mkandarasi huyo akiwa eneo la kazi akiendelea na utekezaji wa agizo hilo la kurudia ujenzi wa barabara hiyo kwenye maeneo yote ambayo yameanza kuharibika kutokana na kujengwa chini ya kiwango.Zinazohusiana;Kafulila azuia malipo kwa mkandarasi CHICCO.

Aidha,mkandarasi huyo ameanza kufunga kwa kamba maeneo yote ambayo yameharibika na kuzuia magari kupita huku akitengeneza Barabara mbadala (Division road) kwa ajili ya magari kupita ambapo maeneo mengine ameanza kutengeneza barabara hizo mbadala.

Pia DIRAMAKINI Blog imeshuhudiwa mkandarasi huyo katika maeneo ambayo amefunga barabara kwa ajili ya kurudia ujenzi, vifaa vyake vimeonekana vikiondoa lami nzima iliyokuwepo na kuanza kuweka lami nyingine mpya.

Ikumbukwe kuwa, mara baada ya kuapishwa na kuwa Mkuu wa mkoa huo, Kafulila kazi yake ya kwanza ilikuwa kufanya ukaguzi kwenye barabara hiyo ambayo ilikuwa imeharibika zaidi na kubaini kuwa imejengwa chini ya kiwango.

Jambo ambalo lilimshangaza zaidi Mkuu huyo wa mkoa ni kuanza kuharibika kwa barabara hiyo ambayo imegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 60, lakini imeanza kuharibika kabla ya ujenzi kukamilika, lakini pia kabla haijafunguliwa.

Wakiongea na DIRAMAKINI Blog baadhi ya wananchi na madereva wanaotumia barabara hiyo wamempongeza mkuu huyo wa mkoa kwa hatua ya kukagua barabara hiyo na kuagiza ujenzi urudiwe.

"Nadhani hii Barabara ilikuwa inamsubiria huyu Mkuu wa mkoa, maana imeanza kuharibika muda mrefu na yeye kabla hajateuliwa, lakini viongozi na wataalamu walikuwepo, bila ya Kafulila kodi zetu wananchi zilikuwa zimeliwa," amesema Joas Jamila dereva.

Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa, Mhandisi Albert Kent, Mkandarasi huyo anarudia ujenzi huo kwa gharama zake mwenyewe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news