Na Anthony Ishengoma, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati ameuagiza uongozi wa Mgodi wa Barrick uliopo Bulyanhulu mkoani Shinyanga kuhakikisha wanatoa miradi yenye mashiko ile inayochangiwa na mgodi huo kwa jamii badala ya kujikita katika masuala madogo kama vile semina na warsha ili wananchi waweze kufaidika na uwepo wa rasilimali hiyo kubwa katika maeneo yao.
‘’Tunataka wawe na miradi mikubwa ambayo ina manufaa kwenye jamii badala ya kuchangia vizawadi vidogo vidogo kama kuchangia madawati hapa na pale na hii hiki ndicho tunachokilenga,"ameongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemoni Sengati.
Dkt. Sengati amesema hayo wilayani Kahama alipofika katika Mgodi wa Twiga Barrick Bulyanhulu kwa lengo la kujionea ni namna gani taasisi za Serikali zilizopo katika mgodi huo zinavyosimamia utaratibu mzima wa uzalishaji wa madini hususani makinikia ambayo kwa sasa yanasafirishwa nje ya nchi baada taratibu zote zinazotakiwa na Serikali kufuatwa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati akikagua makinikia yanayozalishwa na mgodi wa Tigwa Barrick ulioko Bulyanhulu mkoani Shinyanga alipofika mgodini hapa kujionea taratibu zinazotumika katika uzalishaji wa dhahabu na makinikia hayo.
Aidha, Dkt. Sengati ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wawakilishi wa Serikali katika mgodi huo kuwa wazalendo kwa kuhakikisha serikali hapotezi mapato yake, lakini pia kuwakumbusha kuwa serikali itajengwa na watanzania wenyewe na kusisitiza kuwa hizi ndizo rasilimali tulizonazo zitusaidie kujenga Taifa letu.
Mkuu huyo wa mkoa pia amesisitiza kuwa, katika suala zima la ajira na utaalamu viongozi wa mgodi wanapaswa kutumia wataalamu waliopo maeneo ya Shinyanga kwa kuanzia na Wilaya ya Kahama ambapo mgodi unapatikana na kama watashindwa kabisa waangalie maeneo mengine ya Tanzania kwa faida ya kurudisha fadhila kwa jamii.
‘’Hatutegemei vitu vinavyoweza kupatiwa majibu na watanzania vitoke nje, lakini hatutegemia pia vitu vinavyoweza kufanywa na mtu wa eneo la mgodi vifanywe na mtu wa Kahama Mjini wala vitu vinavyoweza kufanywa na mtu wa Kahama Mjini vifanywe na mtu wa Shinyanga mjini au mtu wa Shinyanga atoke Dar es Salaam tunataka matokeo ya mgodi yaanzie hapa Shinyanga,"ameongeza Dkt. Sengati ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kahama wakiangalia kwa makini makinikia yanayozalishwa na mgodi wa Twiga Barrick uliopo Bulyanhulu mkoani Shinyanga alipofika mgodini hapa kujionea taratibu zinazotumika katika uzalishaji wa dhahabu na makinikia hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kahama wakiangalia kwa makini makinikia yanayozalishwa na mgodi wa Twiga Barrick uliopo Bulyanhulu mkoani Shinyanga alipofika mgodini hapa kujionea taratibu zinazotumika katika uzalishaji wa dhahabu na makinikia hayo.
Naye mwakilishi wa Afisa Madini Mkoa wa Shinyanga, Bw. Modest Karmo alimevieleza vyombo vya habari mgodini hapo kuwa, ofisi yake inawawakilishi wanaofanya kazi katika mgodi huo na amemuhakikishia mkuu wa mkoa kwa kumuonyesha taratibu zote za nyaraka na njia zinazotumika katika utaratibu mzima wa uchimabji madini mgodini hapo, lakini pia kumuonesha taratibu zote za udhibiti hadi madini yanapopata kibali cha kusafirishwa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga amekuwa wilayani Kahama kwa ziara ya siku mbili ili kujionea maemdeleo ya wilaya hiyo ambapo awali alitembelea miradi ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje pamoja na jengo la utawala na alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa wadau mbalimbali wa wilaya hiyo.
Tags
Habari