MREMBO ATEULIWA BALOZI WA TAKUKURU MKOA WA DODOMA

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mapambano dhidi ya rushwa ni wajibu wa kila Mtanzania. Wajibu huu ni muhimu kwani rushwa ina athari katika kila sekta ya jamii, na uwepo wake hupindisha haki na kuondoa usawa. 

Mashindano ya urembo ni sanaa yenye umuhimu mkubwa kwa washiriki na taifa kwa ujumla hata hivyo, uwepo wa vitendo vya rushwa katika tasnia hii huondoa usawa na haki na hivyo tunaweza kupata washindi wasio stahili ambao hawataweza kuwa wawakilishi wazuri ndani na nje ya nchi.

Mkoa wa Dodoma upo katika mchakato wa kutafuta mrembo wake ambaye atauwakilisha kwenye mashindano ya urembo ngazi ya taifa. 

Jioni ya Juni 19, 2021, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma ilidhamini usiku wa vipaji kwa washiriki wa shindano la kutafuta mrembo wa mkoa wa Dodoma Miss Dodoma talent show uliofanyika katika Hoteli ya Morena iliyopo Jijini Dodoma. Shindano limeandaliwa na kampuni ya Nikalex LTD.
Washiriki kumi na nne (14) kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dodoma walishiriki ambapo wote walieleza namna wanavyoitambua TAKUKURU, majukumu yake na umuhimu wa umma kushirikiana nayo katika vita dhidi ya rushwa. 

Aidha, walieleza maana ya rushwa na namna ya kutoa taarifa TAKUKURU BURE kwa kutumia simu ya dharura namba 113.

Pamoja na washindani wote kujieleza vyema, Majaji walimchagua mshiriki Subilaga Ambangile kutoka Wilaya ya Mpwapwa kuwa Balozi wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma baada ya kuridhika na kipaji chake cha kuelimisha vijana kuhusu masuala ya rushwa na umuhimu wa kuvunja ukimya na kukataa rushwa ya ngono na aina nyingine. 

Balozi huyo alieleza kwa ufasaha maana ya rushwa na namna ambavyo ina madhara kwenye jamii na akatoa wito kwa wananchi wote kuwa tayari kutoa taarifa za vitendo vya rushwa TAKUKURU hata kama wahusika ni watu wao wa karibu.

Mwisho, tunawasihi wananchi wa mkoa wa Dodoma hasa vijana wa kike na wengineo kuendelea kutupa taarifa pindi wanapokutana na changamoto za rushwa ya ngono sehemu yoyote na tunaahidi kuzifanyia kazi taarifa hizo kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria. RUSHWA HAILIPI.

Imetolewa na:

Sosthenes Kibwengo

Mkuu wa TAKUKURU (M) Dodoma

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news