Rais Dkt.Mwinyi:Ninatambua mchango wa watumishi wa umma

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema anatambua mchango wa Watumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya kuwahudumia wananchi wa Zanzibar.

Dkt. Mwinyi amesema hayo Juni 23, 2021 katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, katika hafla iliofanyika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil, Kikwajuni jijini Zanzibar.

Amesema, watumishi wa Umma wa Zanzibar wana mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko yatakayowezesha kuinua hali ya uchumi wa nchi ili kufikia kiwango cha juu, kama ilivyoelekezwa katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) Waziri wa Katiba,Sheria,Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Haroun Ali Suleiman (wa pili kulia) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa (kulia) Katibu Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji wakisimama kwa pamoja wakati wimbo wa Taifa katika viwanja vya Ukumbi wa Sheikh drisaa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar katika maadhimisho ya tatu ya Wiki ya Utumishi wa Umma Zanzibar hafla iliyofanyika leo.

Amesema, wakati huu wafanyakazi katika ngazi mbali mbali wakiadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma, hawana budi kutafakari na kutathmin hali ya ufanisi katika utumishi wao, akibainisha dhamana waliyonayo katika kuishauri Serikali katika utungaji wa Sera na Sheria.

Amesema, kumekuwepo mafanikio yalioanza kuonekana katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali, ukuaji wa uchumi, kuimarika kwa nidhamu yya matumzii ya fedha za Serikali pamoja na Uwajibikaji.

Hata hivyo Rais Dk. Mwinyi alisema bado kuna safari ndefu kufikia mafanikio yanayohitajika, kwani kuna watumishi wa umma wachache ambao bado hawajabadilika na hivyo kuviza juhudi za kufikia malengo ya ukuzaji uchumi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Akigusia kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Uwajibikaji na Uadilifu katika Utumishi wa Umma ni kichocheo cha kuimarisha utoaji wa huduma katika jamii”, Dk. Mwinyi alisema kauli mbiu hiyo inahimiza na kusisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuongeza kasi ya Uwajibikaji na uadilifu ili kutoa huduma bora na kwa wakti muafaka kwa jamii.

“Taifa lolote ambalo watumishi wake hawawajibiki ipasavyo na wasio waadilifu, maendeleo kwao huwa ndoto na wananchi wataendelea kukosa huduma wazostahili”, alisema.

Aliwashukuru wananachi kwa kumuunga mkono pale anapochukua hatua za kubadili watendaji kwa madhumuni ya kuongeza uwajibikaji na kuleta ufanisi katika kuwatumikia wananchi.

Aidha, aliwataka watumishi wa Umma kuleta mageuzi ya kiutendaji katika Utumishi wa Umma ili kuongeza ufanisi na kuleta tija katika utekelezaji wa wajibu wao na dhamana walizokabidhiwa.

Alisema taarifa na matukio tofauti yaliojitokeza katika siku za hivi karibuni kwa baadhi ya taasisi kubainika kujihusisha na matumizi mabaya ya fedha za umma, wizi na ubadhirifu wa fedha za umma, utekelezaji wa miradi iliyo chini ya viwango pamoja na wizi wa vifaa mbali mbali vya Serikali, yanatoa taswira ya kutokuwepo uadilifu na uwajibikaji kwenye taasisi hizo.

Aliwataka watumishi wa umma kubadilika katika utendaji wao kwa kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kama ilivyoainishwa kwenye sheria mbali mnbali.

Alisema ili kufikia dhamira ya kuleta mabadiliko na mageuzi yatakayoleta ufanisi katika utumishi wa umma, ni lazima kufanyakazi kwa malengo ili kufikia matarajio ya wananchi.

“Twende tukatumie maarifa na taaluma zetu katika kuzitumia rasilimali ziliopo katika taasisi zetu, zikijumuisha fedha na vifaa mbali mbali ili tuweze kuleta ufanisi katika kuwapa huduma bora wanazostahiki wananchi wetu ”, alisema.

Dk. Mwinyi alisistiza umuhimu wa viongozi na watendaji wa taasisi kusikiliza changmoto zinazowakabili wananchi pamoja na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi, huku akiwataka kuepuka urasimu usio na lazima katika utoaji wa huduma.

Alisema tayari kuna mafanikio makubwa yaliofikiwa katika matumizi ya mfumo wa ‘Sema na Rais’ (SNR), na kubainisha kuwepo changamoto kadhaa zilizokwisha kupatiwa ufumbuzi.

Alitoa rai kwa wanachi kutoa taarifa zilizoo kamilika pamoja na kushirikian na viongozi wanaohusika ili taarifa hizo ziweze kufuatiliwa vizuri na kufikia malengo ya kuanzishwa kwa mfumo huo.

Aidha, alisistiza umuhimu wa viongozi kujiongeza na kuleta ubunifu katika taasisi zao, akibainisha baadhi yao kutokuwa na mipango wala mikakati ya maendeleo kisekta katika taasisi wanazoziongoza na kusubiri Ofisi yake (Ikulu) iwapangie mipango hiyo.

Sambamba na hilo, Dk. Mwinyi akataka kuwepo matumizi ya teknolojia ya kisasa katika utumishi wa umma, ikiwa ni hatua ya kupunguza muda wa wananachi kususbiri huduma.

Vile vile, alizitaka taasisi kuwa na nmaadalizi mazuri ya kujua nafasi zitakazoachwa wazi na wafanyakazi wanaotarajiwa kustaafu, ili kuondoa sababu za baadhi ya wataalamu kuombewa muda wa ziada wa utumishi kwa njia ya mikataba.

“Watumishi wanaoelekea kustaafu waandaliwe ili waweze kwenda kuyakabili maisha baada ya kustaafu, wajuilishwe kwa wakati pamoja na kuandaliwa stahili zao mapema ili kuwaondolea usumbufu,”amesema.

Nae, Waziri wa Nchi, (OR) Katiba, Sheria , Utumishi wa umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman aliwataka watumishi wa Umma kurekebisha kasoro mbali mbali zilizojitokeza katika taasisi na maeneo yao ya kazi.

Waziri Haroun alitumia fursa hiyo kumkabidhi tuzo maalum ya heshima Rais Dk. Mwinyi, ikiwa ni hatua ya kuthamini mchango wake mkubwa katika kuimarisha nidhamu , uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma na Utawa bora nchini.

Mapema,Katibu Mkuu Wizara ya Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Seif Shaaban Mwinyi alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa umma mwaka hu, inalenga kuwahamasiha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuimarisha hadhi ya Utumishi wa umma na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Katika hatua nyengine, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mansura Mossi Kassim aliwasilisha mada ya ‘Hali ya Utumishi wa Umma Zanzibar na hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha uwajibikaji na kusema miongoni mwa changmoto kubwa ziliopo ni ile ya kutokuwepo chombo rasmi kinachoratibu mafunzo ya utumishi wa umma, huku kila taasisi ikifanya shughuli hiyo pekee.

Aidha, Katibu Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Asma Hamid Jidawi, akiwasilisha mada ya ‘mchango wa Tume ya Madili ya Viongozi wa Umma’, alisema wajibu wa Viongozi wa umma ni kuzingatia maadili ya Utumishi wa umma, na hivyo akasisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya malezi na elimu hatua kwa hatua ili kuimarisha maadili.

Katika Mkutano huo wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki, wakiwemo Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Talib Mwinyi , Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,Makatibu wakuu, Makatibu Tawala za Mikoa na Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa wadhamini pamoja na watumishi wa umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news