Rais Samia awataka wanawake kuchangamkia fursa za kiuchumi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake kote nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazowasaidia kusukuma mbele maendeleo yao na ya Taifa kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayo dhamira ya dhati ya kuwaunga mkono.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wanawake wa Tanzania katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma leo tarehe 8 June, 2021.

Mhe. Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 08 Juni, 2021 alipokuwa akizungumza na wanawake wa Tanzania kupitia wanawake wa Mkoa wa Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma uliohudhuriwa na zaidi ya Wanawake 8,000.

Mhe. Rais Samia amesema kutokana na takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuonesha kuwa hadi mwaka jana Tanzania ilikuwa na wanawake zaidi ya Milioni 29.4 ambao ni asilimia 51.04 ya watu wote, wanawake ni jeshi kubwa ambalo linategemewa katika uchumi na ustawi wa jamii hivyo hawapaswi kubaki nyuma na badala yake watumie fursa mbalimbali zilizopo kufanya mageuzi yatakayolisaidia Taifa kusonga mbele.

Wanawake mbalimbali nchini wakimshangilia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati akiwahutubia katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma leo tarehe 8 June, 2021.

Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kujenga miundombinu na kuimarisha huduma zitakazowawezesha wanawake kufanya shughuli zao kwa manufaa na tija ikiwemo kujenga miundombinu ya usafiri, elimu, afya, maji na kuwaunganisha na taasisi zinazotoa ujuzi na fedha za kuendeshea biashara

Mhe. Rais Samia ametaja baadhi ya maeneo ambayo Serikali imewawezesha wanawake kiuchumi kuwa ni kuanzisha mifuko 61 ambayo imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi Trilioni 2.22 kwa wanawake Milioni 5.3 na mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 63.489 iliyowafikia wanawake 938,802.

Kuhusu majukwaa ya kuwawezesha wanawake ambayo yeye mwenyewe ameyaanzisha katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji, na ambayo yamewasaidia wanawake wengi kuanzisha vyama vya akiba na mikopo, Mhe. Rais Samia ametaka viongozi wa ngazi husika wahakikishe majukwaa hayo yanakuwa na uhai na kwamba yeye mwenyewe atayatupia macho.

Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa wanawake wote nchini, kukaa na kutafakari maeneo ambayo wanafanya vizuri na maeneo ambayo hawafanyi vizuri ili kuchukua hatua za kurekebisha dosari na amewata Mawaziri wenye dhamana za afya, elimu na Serikali za Mitaa kushughulikia changamoto za Wanawake ili kurahisisha shughuli zao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimtunza Msanii wa Taarabu Sabah Salum Muchacho wakati akitumbuiza katika mkutano wa Wanawake wa Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma leo tarehe 8 June, 2021. (PICHA NA IKULU).

Amewahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha inatekeleza ipasavyo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ikiwemo kuhakikisha usambazaji wa maji Mijini unafikia asilimia 95 na Vijijini asilimia 85, kujenga miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo ujenzi wa reli na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato Mkoani Dodoma.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka wanawake kote nchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira ambayo ni muhimu katika utatuzi wa changamoto ya maji, kuhamasika kutumia mifumo ya kidijitali na amezialika taasisi na mashirika mbalimbali ya binafsi na Serikali kujitokeza kuwawezesha wanawake wa Tanzania.

Katika risala ya wanawake, iliyosomwa na Bi. Joyce Kashozi wanawake hao wamemshukuru Mhe. Rais Samia kwa namna anavyowaamini wanawake na kuwapa nafasi nyingi za uongozi na wamemuahidi kutomuangusha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news