Rais Samia: Serikali itakuwa bega kwa bega na Sekta binafsi nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwa kuendelea kulisimamia Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) ili kukuza na kujenga uchumi ambao utanufaisha Watanzania wote.Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia katika Ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC)uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo. Kushoto ni Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa.

Akihutubia katika Ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Baraza hilo lenye kauli mbiu ya “Ufanisi wa Biashara na Uwekezaji katika Uchumi wa Kati Tanzania uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema kuwa sekta binafsi ni muhimili mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi yeyote duniani, kwa hiyo kupitia Baraza hilo serikali itaendelea kuipa kipaumbele sekta binafsi.

"Ni ukweli usiopingika kwamba Sekta Binafsi ni muhimili mkubwa wa maendeleo na kuna usemi mwingine kuwa sekta binafsi ni injini ya kukuza uchumi, kwa hakika dunia ya leo hakuna taifa lolote duniani linaloweza kujinasua kiuchumi bila kufanya kazi bega kwa bega na sekta binafsi, Serikali itaendelea kutoa ushrikiano kwenu,"amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema kuwa, Serikali ilianzisha Baraza la Bisahara mwaka 2001 na sasa ni miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, na linatumika kama jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na Sekta Binafsi ili kutoa nafasi ya kila upande kutoa mawazo na kuboresha sera, sheria na kanuni katika sekta ya uwekezaji na biashara.

Aidha, Rais Samia alisema kuwa TNBC ni jukwaa la kuwaleta wadau wa biashara ya uwekezaji pamoja na Serikali katika uelewa wa pamoja kuhusu masuala muhimu ya maboresho ya mazingira ya biashara hasa kwenye mabadiliko ya Sera, Sheria na Kanuni ambazo zitaleta fursa kubwa wafanyabiashara kwenye sekta zote.

Akibainisha mchango wa TNBC katika kukuza uchumi, Rais Samia alisema kuwa hilo ni Baraza na jukwaa kubwa ambalo kila mfanyabiashara anapata utaratibu wa biashara na uwekezaji ili kukuza mitaji na kuchangia uchumi wa taifa kwa kutoa kodi.

"Baraza hili limekuwa chachu ya kuboresha na kuanzisha Sera, Sheria, Kanuni na taratibu za biashara na uwekezaji nchini, tumejionea leo kulikuwa na mambo mengi ya mafanikio na changamoto ambazo zimetajwa hapa na Mwenyekiti wa Sekta binafsi ambayo tunayaangalia kwenye Sera, Sheria na Kanuni na ni ahadi yangu ni kuwa tunakwenda kuyaangalia kwa pamoja sisi na Sekta Binafsi,"amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa, TNBC limekuwa na mafanikio makubwa ikwemo kuanzishwa kwa mabaraza ya Mikoa na Wilaya ambapo ametumia fursa hiyo kuwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kutoa ushirikiano kwa wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na uongozi wa juu wa TNBC kwani wao ndiyo wenyeviti wa mabaraza hayo.

Rais Samia alitumia Fursa hiyo kuwashukuru Watangulizi wake katika kufanikisha kuanzishwa kwa baraza hilo na kusimamiwa ambapo ameahidi kuwa baraza litaendelea kufanya kazi na kusimamia uboreshwaji wa mazingira ya biashara hasa kwa wafanyabiashara wanawake ili waweze kukuza uchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Sekta Binafsi (TPSF) Bi. Angelina Ngalula amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa pamoja na wawekezaji.

"Naomba nikupongeze Mhe. Rais, kutokana na uamuzi wako ulioufanya katika kuboresha mazingira ya Biashara na kuipa kipaumbele sekta binafsi, kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya sekta binafsi na Serikali katika majadiliano na kutoka na mawazo wezeshi kwa utekelezaji wa biashara,"amesema Bi. Ngalula.

Alibainisha kuwa ndani ya muda wa mwezi mmoja Serikali imejidhatiti kuwasikiliza wafanyabiashara kupitia Taasisi ya Sekta binafsi, kwani wamefanya mikutano kadhaa na serikali ukiwemo ule wa Waziri Mkuu, Wizara ya Kilimo uliofanyika Mkoani Singida ukilenga kujadili mikakati ya uzalishaji mbegu za alizeti na kukuza kilimo cha zao hilo.

Aidha, Bi. Ngalula alimpongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa usimamizi madhubuti wa mazao ya kimkakati hususan mchikichi, alizeti na mazao mengine ambayo sekta binafsi inahusika kuwekeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news