NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Lengai Ole Sabaya (34) na walinzi wake wamepelekwa Mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo lililopo nje kidogo ya Jiji la Arusha kwa tuhuma za kutenda makosa mbalimbali ambayo hayana dhamana.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa mbalimbali likiwemo la uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kupokea rushwa.
Hatua hiyo inakuja zikiwa zimepita siku chache baada ya Lengai Ole Sabaya kusimamishwa kazi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Mei 13, 2021 ili kupisha uchunguzi kwa tuhuma ambazo zinamkabili.
Sabaya amefikishwa mahakamani hapa mchana akiwa amefungwa pingu na baada ya wote kushuka kwenye magari ya polisi walitakiwa kuchuchumaa na kisha kupelekwa katika chumba maalum na baadaye kuingizwa mahakamani ili kuruhusu taratibu zingine ziendelee.

Aidha, Kweka amesema, Lengai Ole Sabaya na wenzake watano anatuhumiwa kwa makosa ya kuunda genge la uhalifu, uhujumu uchumi, kujipatia fedha kwa njia ya rushwa na utakatishaji fedha ambapo Sabaya alijipatia shilingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara, Francis Mroso mkazi wa kwa Mromboo ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi ili amsaidie jambo ambalo ni makosa.

Watuhumiwa hao wanadaiwa walimfunga pingu na kumpiga Bakari Msangi ambaye ni Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Sombetini na kumuibia shilingi 390,000.
Aidha, huko eneo la Bondeni jijini Arusha wakitumia silaha, Lengai Ole Sabaya na walinzi hao wanatuhumiwa kumpiga, kumtishia silaha na kumpora Ramadhani Ayoub simu na shilingi 35,000, kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Juni 18, mwaka huu mahakamani hapo.
Tags
Habari