Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi ,George Simbachawene amesema pamoja na Serikali kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa hapa nchini, watumiaji wa dawa hizo wamebuni mbinu mbadala ya kutumia dawa za hospitali za usingizi na kemikali bashirifu kama kilevi.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma wakati alipomwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Dawa za Kulevya Duniani iliyoenda sambamba na kauli mbiu tuelimishane kuhusu tatizo la dawa za kulevya kuokoa maisha.
Amesema kuwa, takwimu zinaonesha juhudi kubwa zimefanyika kupanua vituo vya tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya huku akisema Serikali imejizatiti kuanzisha vituo vingi katika maeneo yote yaliyoathirika ili waathirika wengi waweze kupatiwa matibabu.
"Ni jukumu la kila mmoja wetu kupambana na dawa za kulevya ili kulinda afya zetu huku mkitoa taarifa kwa wanaojihusisha na biashara hizo ili kuchukuliwa hatua, mshiriki kikamilifu kuelimisha mbinu sahihi za kuepuka kwenye vishawishi vya dawa za kulevya.
"Vijana wengi wa kiume wamekuwa wakiwaaminisha vijana wa kike kwamba wanapotumia dawa za kulevya katika mapenzi yatanoga na kupata starehe jambo ambalo sio kweli na wanatembea na madawa hayo kwenye magari yao, hivyo niwatake maaskari wetu hakikisheni mnaposimamisha magari myakague,"amesema Simbachawene.
Amesema kuwa, matumizi hayo ya dawa za kulevya yana madhara mengi hasa kupoteza nguvu kazi,uharibifu udokozi pamoja na magonjwa mbalimbali ya ini, moyo na kuambukiza virusi vya ukimwi wale wanaojidunga sindano.
Aidha, ameongeza mamlaka husika kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa vyombo vya habari hapa nchini kwa kuwapa semina mbalimbali kwani wamekuwa mstari wa mbele kutangaza madhara ya dawa za kulevya.
"Niitake Wizara ya Elimu kuhakikisha inaboresha elimu ya dawa za kulevya kwenye mitaala ya shule za misingi na sekondari hadi vyuo ili kuwawezesha vijana wa kitanzania kupata elimu sahihi kuhusu dawa za kulevya pamoja na kuwafundisha stadi za maisha,"amesema.
Hata hivyo, amezitaka taasisi za kidini kuendelea kukemea dawa ya kulevya wawapo katika nyumba za ibada kwani kupitia wao jamii inawasikiliza.
Antoni Machael ambaye ni miongoni mwa vijana waathirika wa dawa za kulevya akizungumza na DIRAMAKINI Blog amewasihi vijana kutokujihusisha na biashara hiyo hatari ambayo licha ya kuwapotezea malengo pia inaweza kuyaangamiza maisha yao.
Tags
Habari