Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog
KUELEKEA Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani 2022 jamii imetakiwa kuacha tabia ya kuwaficha watu wenye ulemavu ili kuiwezesha Ofsi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kupata taarifa sahihi za kundi hilo zitakazotumika kutekelezea mahitaji yao kwa ufanisi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha wataalamu kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Amesema kuwa, kutokana na kutokuwepo kwa takwimu sahihi za watu wenye ulemavu imekuwa sababu kubwa kwa Serikali kushidwa kutimiza mahitaji ya kundi hilo.
Pia amesema kuwa, kitendo cha jamii kuwaficha watu wenye ulemavu wakati wa kipindi cha Sensa ya Watu na Makazi wanaikosesha Serikali fursa ya kupata takwimu sahihi ambazo zingetumika kuwasaidia katika kero mbalimbali zinazaowakabili.
“Maelekezo ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan anasema kuwa walemavu bado wana shida nyingi sana, lakini hili linasababishwa na sababu kubwa ya kukosekana kwa takwimu sahihi, hivyo tushirikiane katika Sensa ya 2022.
“Pia kupata takwimu sahihi za idadi ya walemavu katika maeneo yote na aina ya ulemavu wao ili kuweza kuzishughulikia ipasavyo changamoto zao,”amesema.
Aidha, amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu katika Sensa ya watu na makazi mwakani imetenga bajeti ambayo itatoa suluhu ya upatikanaji wa takwimu sahihi ya idadi ya watu wenye ulemavu nchini.
Kadhalika, amesema kuwa kama ambavyo Umoja wa Mataifa unaagiza kuwa hakuna kumwacha mtu nyuma ni jukumu la taifa kuhakikisha kila kundi linahusishwa katika zoezi hilo la Sensa ya watu na makazi mwakani.
“Pamoja na maagizo hayo, lakini pia sisi kama taifa tumeridhia mikataba mbalimbali ya kulinda haki za watu wenye ulemavu, lakini pia zipo sera pamoja na sheria za nchi ambazo tunatakiwa kuzilinda,”amesema.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa, katika Sensa ya watu na makazi ya mwakani, wamejipanga kuhakikisha kila kundi linajumuishwa ili kuwa na takwimu sahihi kwa ajili ya kulisaidia Taifa kutekeleza majukumu yake.
“Zoezi lililopo mbele yetu ni la kitaifa na linashirikisha makundi yote, NBS tutahakikisha kuwa makundi yote katika jamii yanashirikishwa ili kupata takwimu sahihi,”amesema Dkt.Chuwa.
Vile vile, amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kundi la watu wenye ulemavu ni kubwa hasa kwa nchi zinaendelea na hasa katika bara la Afrika.
“Kwa bara la Afrika idadi ya watu wenye ulemavu ni asilimia 40, hivyo tunahitaji mipango imara,”amesema.
Tags
Habari