NA MWANDISHI DIRAMAKINI Blog
ASANTE kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa viongozi waliopewa maono haya chanya akiwemo Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kwa kuona mbali kuhusu kuwekeza katika miradi kabambe ya kimkakati kwa ajili ya uzalishaji wa umeme.
Kila mmoja kushukuru ndiyo hatua ya kwanza, kwani tulishuhudia namna ambavyo miradi mingi ya nishati ilivyopigwa vita nchini wakiwemo wanaharakati wa mazingira Duniani kuelekeza lawama kwetu, lakini viongozi wetu wakasimama kidete, kabla ya kuiangazia ripoti ya mashirika matano ya Umoja wa Mataifa inayoangazia changamoto kuhusu umeme duniani, MWANDISHI DIRAMAKINI anakupitisha huku, twende pamoja.
Ipo hivi, Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kufanikisha utekelezaji wa sera ya viwanda hususani kupitia miradi ya nishati ya umeme.
Serikali imeweka kipaumbele cha kusimamia utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Nyerere katika Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge). Mradi huu ni njia sahihi ya kufikia Uchumi wa Viwanda ifikapo mwaka 2025.
Hafla ya Utiaji saini ya Mkataba wa Ujenzi wa Mradi ilifanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania tarehe 12 Desemba, 2018 na kushuhudiwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa Misri, Dkt. Mostafa Madbouly.
Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Magufuli alisisitiza Serikali ya Awamu ya Tano ipo imara na itahakikisha kuwa mradi huo utakaozalisha zaidi ya Megawati 2100 unakamilika kwa wakati ili kuiwezesha Tanzania kuweza kupiga hatua kubwa zaidi katika maendeleo.
Pia wakati huo Rais alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuharakisha utekelezaji wa mradi wa umeme wa Nyerere huo kutokana na ukweli kuwa uzalishaji wa umeme kwa chanzo cha maji ni rahisi katika uzalishaji wake ukilinganisha na vyanzo vingine vya uzalishaji wa nishati ya umeme ikiwemo upepo, makaa ya mawe, nyuklia, jua na joto ardhi.
Vilevile, Waziri wa Nishati, Mheshimiwa. Dkt. Medard Kalemani (Mb) aliongeza kuwa kupitia katika vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme vilivyopo nchini, Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuhakikisha Tanzania inaweza kuzalisha Megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 na hivyo kuiwezesha nchi kuwa muuzaji wa umeme katika nchi jirani.
Mradi huu unajengwa na mkandarasi wa kampuni ya Arab Contractor kutoka Misri utagharimu kiasi cha Trilioni 6.5 na unatarajiwa kujengwa kwa kipindi cha miezi kati ya 36 mpaka 42 ya ukamilishaji wa mradi huo.
Kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi, kutaiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kitachokasaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa uchumi wa viwanda na mradi wa reli ya kisasa, hatua itakayoiwezesha kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wake.
Miradi Mingine ya Umeme
Mbali na mradi huo pia kuna miradi mingine kabambe ukiwemo Mradi wa Msongo wa kV 400, North - West, Mradi wa msongo wa kV 400 na Kv 220, North –East Grid ( DarTanga-Arusha), Mradi wa njia ya kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kv 220 ya Geita-Nyakanazi,Mradi wa Msongo wa Kv 220 Bulyanhulu - Geita na Geita – Nyakanazi pamoja na matumizi ya gesi asilia.
RIPOTI
Jitihada hizo ambazo zimeungwa mkono kwa nguvu moja na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ndizo zinaendelea kuifanya Tanzania ambayo inatarajia kukamilika kwa miradi hiyo karibuni kuibuka kinara katika uzalishaji wa umeme wa kutosha.
Umeme ambao, Mheshimiwa Rais Samia wakati akizungumza na wanawake wa Tanzania kupitia wanawake mkoani Dodoma Juni 8, mwaka huu amesisitiza kuwa ifikapo mwaka 2024, vijiji vyote Tanzania vitakuwa na nishati ya umeme kwa ajili ya kuwapa fursa wananchi kuitumia nishati hiyo kwa matumizi ya nishati na kuongeza fursa za uzalishaji.
Hatua hiyo, inaipa kisogo ripoti mpya iliyotolewa na mashirika ya kimataifa likiwemo la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), Shirika la Kimataifa Linalohusika na Nishati Jadidifu (IRENA), Idara ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi na Maendeleo (DESA), Benki ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) ambayo imeeleza kuwa, idadi ya watu wasio na nishati ya umeme Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika imeongezeka.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa,hayo yanajiri wakati ambapo katika muongo mmoja uliopita idadi kubwa ya watu duniani wamepata fursa ya nishati ya umeme kuliko wakati mwingine wowote.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo inayofuatilia hatua zilizopigwa katika utimizaji wa lengo Namba 7 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa linalohusu nishati, imeonya kwamba endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa nishati ya umeme basi Dunia haitaweza kutimiza lengo la kuhakikisha fursa ya kuwa na nishati ya gharama nafuu, ya kuaminika na endelevu kwa wote ifikapo mwaka 2030.
"Lazima pengo la usawa katika nishati lizibwe na suluhu endelevu zipatikane zikilenga nchi za Afrika ambazo zimeachwa nyuma katika lengo la kimataifa la fursa ya kimataifa ya nishati kwa wote,"imebainisha ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti katika miaka 10 iliyopita tangu mwaka 2010, hatua zimepigwa katika ufikiaji wa lengo namba 7 la nishati lakini hatua hizo hazipo sawa katika kanda mbalimbali.
Pia kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu zaidi ya bilioni moja walipata fursa ya nishati ya umeme duniani kote, lakini wakati huo huo watu milioni 30 wengi wakiwa kutoka katika mataifa ya Afrika athari za janga la virusi vya Corona (COVID-19) zimefanya washindwe kumudu huduma za nishati ya umeme.
Aidha,nchi zinazoongoza kwa kutokuwa na fursa kubwa ya nishati hiyo ni Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Ethiopia ambayo sasa imeiangusha India na kushika namba tatu duniani kwa kukosa nishati hiyo muhimu.
Duniani kote ripoti inaeleza kuwa, idadi ya watu wasiokuwa na huduma ya umeme ilipungua kutoka bilioni 1.2 mwaka 2010 hadi milioni 759 mwaka 2019.
Huduma za umeme kupitia suluhisho jadidifu zinazidi kushika kasi. Idadi ya watu waliounganishwa na gridi ndogo imeongezeka zaidi ya mara mbili kati ya 2010 na 2019, kutoka watu milioni 5 hadi watu milioni 11.
Lakini, chini ya sera za sasa ilizopangwa na athari kubwa za janga la COVID-19, watu wanaokadiriwa kuwa milioni 660 bado hawatakuwa na fursa ya nishati hiyo ifikapo mwaka 2030, na wengi wao wakiwa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Wakati huo huo, watu wengine bilioni 2.6 walibaki bila nishati safi ya kupikia mwaka 2019, ikiwa ni theluthi moja ya idadi ya watu wote ulimwenguni.
Udumavu mkubwa wa maendeleo ya upatikanaji wa nishati hiyo tangu mwaka 2010 husababisha mamilioni ya vifo kila mwaka kutokana na matatizo ya kupumua yanayosababishwa na moshi wa kupikia na bila hatua za haraka za kuongeza nishati safi ya kupikia Dunia itapungukiwa katika kutimiza lengo lake kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.
Hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ilielezwa kuwa, ongezeko la idadi ya watu ni kubwa kuliko fursa ya kufikia nishati hiyo, hivyo watu milioni 910 katika ukanda huo wanakosa nishati safi ya kupikia.
Nchi 20 za juu zenye upungufu mkubwa wa nishati hiyo zinashikilia asilimia 81 ya idadi ya watu duniani ambao wanaishi bila kupata mafuta safi na teknolojia. Kati ya hizo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ethiopia, Madagaska, Msumbiji, Niger, Uganda na Tanzania (kwa juhudi za sasa za Tanzania, tunakwenda kutoka hapa) walikuwa na idadi ya chini au sawa na asilimia tano ya watu wao ndio walio na fursa ya kupata nishati safi ya kupikia.
Na katika upande wa Habari njema Indonesia, Cambodia na Myanmar wanapiga hatua kila mwaka katika kipindi chote cha uandishi na tathimini ya ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inachunguza njia anuwai za kuziba pengo hilo ili kufikia SDG7, na moja ya njia kubwa ni kuongeza kiwango cha matumizi ya nishati jadidifu ambazo zimethibitisha ustahimilivu kuliko sehemu zingine za sekta ya nishati wakati wa janga la COVID-19.
Wakati nishati jadidifu au mbadala imeshuhudia ukuaji ambao haujawahi kutokea katika muongo mmoja uliopita, sehemu kubwa ya matumizi ya nishati ilibaki kuwa thabiti wakati matumizi ya nishati ya ulimwengu yalikuwa kwa kiwango sawa.
Nishati jadidifu zina nguvu zaidi katika sekta ya umeme, zilifikia karibu asilimia 25 mwaka 2018, wakati maendeleo katika sekta ya kupasha joto na uchukuzi yamekuwa polepole sana.
Zaidi ya theluthi moja ya ongezeko la uzalishaji wa nishati mbadala mwaka 2018 inaweza kuhusishwa na Asia ya Mashariki inayochangiwa na unyakuzi mkubwa wa nishati ya jua au sola na ya upepo nchini China.
Maendeleo makubwa zaidi ya kiwango cha nchi katika nishati mbadala kwa mwaka 2018 yalionekana nchini Uhispania, kwa sababu ya uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji, ikifuatiwa na Indonesia ambapo uzalishaji wa haraka wa nishati itokanayo na kinyesi imebeba jukumu kubwa.
Ili kuongeza kwa kiasi kikubwa sehemu ya nishati mbadala kulingana na lengo la SDG 7, juhudi za sasa zinahitaji kuharakishwa katika sekta zote za matumizi ya nishati hiyo kwa watumiaji katika mahitaji ya jumla ya nishati.
Uboreshaji wa kiwango cha nishati (wakala wa ufanisi wa nishati) unasonga mbali zaidi kutoka kwenye lengo lililowekwa la SDG7 kufikia 2030.
Kiwango cha uboreshaji wa nishati ya msingi ulimwenguni mwaka 2018 kilikuwa asilimia 1.1 ikilinganishwa na 2017, kikiwa ni kiwango cha chini cha wastani cha maboresho tangu 2010.
Uboreshaji wa kila mwaka hadi 2030 sasa utahitaji wastani wa asilimia 3 ikiwa tunataka kufikia lengo imesema ripoti.
Kuongeza kasi ya maendeleo katika kanda na viashiria vyote itahitaji kujitolea kwa nguvu kwa kisiasa, mipango ya muda mrefu ya nishati, sera za kutosha na motisha ya kuongeza kasi ya utafutaji wa suluhu endelevu za nishati.
Mtiririko wa kifedha wa kimataifa kwa umma kwenda nchi zinazoendelea ili kusaidia nishati safi ulifikia dola bilioni14 mwaka 2018, ukiwa umepungua kwa asilimia 35 kutoka kiwango cha juu kabisa cha dolabilioni 21.9 mwaka uliotangulia.
Ripoti inasemka lakini, mwenendo wa jumla wa mtiririko wa kifedha kwa umma umekuwa mzuri katika muongo mmoja uliopita, na kuongezeka mara tatu katika kipindi cha kati yam waka 2010-18 ikionekana kuwa na wastani wa ongezeko kwa miaka mitano.
Mwenendo huu, hata hivyo, unaficha mapengo muhimu ya usambazaji, na ahadi za kifedha zimejikita katika nchi chache na kwa hivyo kushindwa kufikia wengi wale wanaohitaji zaidi msaada wa kimataifa.
Nchi 46 zilizo na maendeleo duni zaidi (LDCs) zilipokea asilimia 20 tu ya msaada wa kifedha wa umma kwa kipindi cha kati ya mwaka 2010-18 na jumla ya dola bilioni 2.8 mwaka 2018 kiwango sawa na cha mwaka 2017 lakini chini kuliko kiwango cha mwaka 2016 na 2015.
Msaada wa kifedha wa kimataifa unahitaji kuongezwa zaidi na kulenga zaidi nchi hizo ambazo ziko nyuma zaidi kufikia lengo la SDG 7.
Katikati ya janga la COVID-19, ambalo limeongeza sana mtazamo wa hatari ya wawekezaji na kuhamisha vipaumbele vya ufadhili wa umma katika nchi zinazoendelea, msaada wa kimataifa wa kifedha kwa umma ni muhimu zaidi kuliko hapo awali ili kukuza viwango vya uwekezaji vinavyohitajika kufikia SDG 7, ripoti inasisitiza.
Tags
Makala