Tanzania yasaini mkataba mkopo wa Bilioni 361.7/- kufanikisha umeme jua

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imesaini mkataba wa mkopo nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130 sawa na shilingi bilioni 361.71 kati yake na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi wa mitambo ya umeme wa jua,anaripoti DOREEN ALOYCE (Diramakini) Dodoma.

Hatua hiyo imefikiwa Juni 11, mwaka huu jijini hapa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba ambapo amesema mradi huo ni wa mwaka mmoja ambao unatarajiwa kuanza mwezi Machi, 2022 na kukamilika ifikapo Machi 2023.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali,Emmanuel Tutuba na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier wakibadilishana hati za mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130.

Katibu Mkuu huyo amesema,ni kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa jua kiasi cha Megawatt 150 katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga huku ukitarajiwa kuwa wa awamu mbili ambapo utaanza na awamu ya kwanza itakayoweza kuzalisha Megawatt 50.

"Sehemu za mkopo huu zitatumika kuboresha na kuimarisha Gridi ya Taifa kuifanya ya kisasa kuweza kujumuisha umeme wa nishati jadilifu zenye muda maalum na pia kupunguza upotevu wa umeme.

"Nafahamu kuwa AFD ilitoa msaada wa kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huu na kuwa kiasi cha Euro laki 7 kimetengwa na Serikali ya Ufaransa kama msaada wa kitaalam katika mradi huu,"amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Dkt.Titus Mwinuka amesema, faida kubwa ya mradi huo itaongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme ili kuwezesha shirika hilo kutimiza malengo ya kuzalisha umeme kupitia vyanzo mbalimbali kwa kutumia nishati jadidifu.

Dkt.Mwinuka ameeleza kuwa, kutokana na mradi huo kutapunguza utegemezi wa umeme wa nguvu za maji wakati wa jua hivyo kuwa na uwezo wa ziada wa uzalishaji ambao utatumika majira ya mahitaji makubwa ya umeme na wakati wa ukame.

"Kwa Mkoa wa Shinyanga,nyongeza ya Megawatt 150 ya umeme wa jua pindi mradi utakapokamilika utawezesha upatikanaji wa umeme katika migodi ya dhahabu na pia kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme wa Gridi ya Taifa na kuchochea maendeleo ya kijamii na uchumi,"amesema.

Naye Balozi wa Ufaransa nchini hapa, Frederic Clavier ameeleza kuwa nchi hiyo inajivunia ushirikiano wa kirafiki na Tanzania na kwamba mkopo huo ni ushuhuda wa kuendeleza ushirikiano wa kimaendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Balozi huyo amefafanua kuwa, utekelezaji wa mkopo huo utasaidia kuchochea uchumi shindani ulio shirikishi,kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji wa huduma za kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news