TARI yazindua Kituo Mahiri cha Usambazaji wa Teknolojia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Morogoro

Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Mheshimiwa Mathayo Maselle kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigella.

Katika hotuba ya ufunguzi, Mheshimiwa Maselle aliwapongeza TARI kwa kuja na mkakati shirikishi wa Usambazaji wa teknolojia za utafiti.

Aidha, alipongeza uwepo wa mbegu bora za mazao yanayostawi katika ukanda wa mashariki mikoa ya Morogoro, Tanga, Pwani na Dar es Salaam.

Hivyo, Wakulima na maafisa ugani wakitumie Kituo hicho kama shamba darasa kuongeza uzalishaji na tija wa mazao ya Kilimo.
Wakati akimkaribisha Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Geoffrey Mkamilo, alieleza kuwa, TARI ina Watafiti wenye uwezo mkubwa wa kutafiti na kugundua teknolojia nyingi mbalimbali.

Hivyo, TARI imejizatiti kuhakikisha Teknolojia hizo zinawafikia watumiaji. Njia mojawapo ya kuwafikishia teknolojia Wakulima na Wadau wengine ni kupitia vituo mahiri vya Usambazaji Teknolojia.

Dkt. Mkamilo aliongeza kuwa Kituo cha Usambazaji Teknolojia kilichopo katika uwanja wa Nane Nane wa Mwl. J.K. Nyarere kilichozinduliwa kitaendelea kutumika Mwaka mzima, ambapo Wakulima, na maafisa ugani watakuwa wanatumia Kituo hicho kujipatia mafunzo ya mbinu Bora za kuongeza uzalishaji kwa tija, Kilimo biashara na lishe bora.

Shughuli ya uzinduzi wa Kituo mahiri Cha Usambazaji Teknolojia cha Mwl. J.K. Nyarere, Morogoro ilishirikisha Wakurugenzi, Mameneja na Watafiti kutoka TARI Makao Makuu, Vituo vya Utafiti vya TARI Mlingano (Tanga), TARI Ilonga (Kilosa), TARI Kibaha (Pwani), TARI Mikocheni (Dar es Salaam) na TARI Ifakara (Morogoro). Washiriki wengine walikuwa Wawakilishi kutoka Sekretariati ya Mkoa wa Morogoro, Maafisa Ugani na Wakulima.

Aidha, Washiriki wengine ni Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ambazo ni miongoni mwa Taasisi za Wizara ya Kilimo zinazoshirikiana kwa karibu na TARI kuhakikisha mbegu Bora zinawafikia Wakulima. Makampuni ya Mbegu yaliyoshiriki ni pamoja na Seed co.

Wakulima walioshiriki katika uzinduzi wa Kituo mahiri Cha usambazaji teknolojia walipata nafasi ya kuzungukia vipando na kupata maelezo kutoka kwa wataalam wa TARI. Wengi walipongeza TARI na Serikali kwa uamuzi wa kuja na teknolojia karibu na wananchi.

Hadi sasa TARI ina vituo viwili vinavyofanya Kazi ya usambazaji wa teknolojia za Kilimo mwaka mzima. Kituo cha kwanza kilichoanza kufanyakazi mwaka 2020 ni Nyakabindi katika mji wa Bariadi, mkoa wa Simiyu na Mwl. J.K. Nyerere mjini Morogoro. Vituo vingine ambavyo vitafuatia kuzinduliwa ni Nzuguni (Dodoma) na Fatma Mwasa (Tabora).

Maandalizi yanaendelea ili kuhakikisha vituo zaidi vya usambazaji teknolojia katika viwanja vyote vya Nane Nane vinafanya Kazi Mwaka mzima.

Imetolewa na Dr. Richard Kasuga, Meneja wa Mawasiliano ya Habari na Menejimenti ya Maarifa, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news