NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Taasisi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP imesikitishwa na kitendo cha kutolewa nje kwa mbunge wa Momba Condester Sichwale kwa madai ya kuvaa mavazi yaliyo kinyume na Kanuni na Taratibu za Bunge.
TGNP Mtandao imesema kitendo hicho ni cha kumdhalilisha mbunge huyo ambaye ni kioo na hamasa kwa wanawake wengi viongozi na wenye nia ya kuwa viongozi.
Mbunge wa Momba Condester Michael Sichalwe akitolewa ndani ya ukumbi wa bunge jana.
Akizungumzia tukio hilo mkurugenzi mtendaji wa TGNP Mtandao amesema, wanaamini kuwa bunge linaongozwa na Kanuni na Sheria ambazo zimebainishwa wazi namna ya kuwawajibisha wabunge ambao watakiuka kanuni na sheria hizo, ikiwemo Spika kujiridhisha kumtoa nje Mbunge kama ilivyoelezwa katika ibara ya 149 ya kanuni za kudumu za Bunge.
Kwa upande wake afisa Programu TGNP Mtandao, Jackson Malangalila kwa upande wake amesema kupitia kitendo cha mbunge Sichwale kuondolewa bungeni kwa sababu ya madai ya mavazi inaonyesha ni tendo linalo endelea kukandamiza nafasi ya mwanamke .
Aidha, TGNP imetoa wito kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania akiwa ni kiongozi wa Bunge kutumia busara na hekima na kuzingatia kanuni katika kukabiliana na matukio kama hayo bungeni ili kuhakikisha haki na usawa vinasimamiwa na kuzingatiwa bungeni kwa manufaa mapana ya taifa.
Ikumbukwe kuwa mbunge wa Momba Condester Sichwale (CCM) jana alitolewa bungeni kwa madai ya kuvaa mavazi yasiyo na staha katika Bunge hilo.
Tayari baadhi ya wabunge wameonekana kuchukizwa na kitendo hicho akiwemo mbunge wa Nyasa Mhandisi Stela Manyanya na Jacklin Ngonyani waliomba muongozo wa spika kwa madai mbunge aliyetolewa nje alionewa.Soma hapa, Mbunge atimuliwa bungeni kwa suruali ya kuwatega waheshimiwa
Tags
Habari