UWT BUTIAMA WAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA KWA KUTEMBELEA NYUMBA SALAMA, WAGAWA ZAWADI

NA FRESHA KINASA

KATIKA kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa Juni 16 kila mwaka, Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara imeungana na Mabinti wa Kituo cha Nyumba Salama kilichopo Kiabakari kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kuadhimisha kwa pamoja. 

Ambapo jumuiya hiyo, imeitaka jamii kutokuwa chanzo cha kuwafanya watoto waishi maisha yasiyo ya furaha na amani kwa kuwafanyia vitendo vya kikatili kuanzia ngazi ya familia.
Sehemu ya mabinti wa Nyumba Salama Kiabakari Butiama Mkoa wa Mara wakiwa wamebeba bango katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Kituo hicho na kuhudhuriwa na UWT Wilaya ya Butiama ambapo pia walipewa zawadi mbalimbali.

Aidha jumuiya hiyo mbali na kushiriki maadhimisho ya Mtoto wa Afrika katika Kituo hicho, wameweza kuwapa zawadi mbalimbali mabinti wanaoishi katika Kituo hicho ikiwemo, sabuni za unga, sabuni za Miche, taulo za kike, vinywaji (soda) mafuta ya kupikia na mchele kama ishara ya upendo na kuwatia moyo katika changamoto walizopitia.

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara, Annastazia Jonathan akizungumza katika hafla hiyo Juni 16, 2021 amesema kuwa, wapo baadhi ya wazazi wamekuwa chanzo cha kuwafanyia ukatili watoto wao jambo ambalo linafifisha juhudi za Serikali katika kumaliza vitendo vya Ukatili wa kijinsia. 

Hivyo amesisitiza jamii kupaza sauti kuwafichua wanaojihusisha na kuwanyanyasa Watoto, kuwapiga, ama kuwatumikisha kinyume cha sheria za nchi.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Butiama, Anna Jonathan akiwakabidhi zawadi mabinti wa Nyumba Salama Kibakari Butiama walipofika kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Butiama Anna Jonathan akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara. Ambapo pia UWT walitoa zawadi mbalimbali kwa mabinti hao. 

Pia wamempongeza Rhobi Samwelly kwa kazi nzuri anazofanya, kwani shirika hili limekuwa na mchango mkubwa sana kuwasaidia watoto kuwaendeleza kimasomo na katika stadi mbalimbali. 

"Niombe ukatili wa kijinsia upigiwe kelele na kila mmoja lengo ni kuwa na Taifa imara ambalo Watoto watajengwa kuanzia ngazi ya familia,"amesema Anna.

Pia, amewaomba wanawake kuwa mstari wa mbele katika kusimamia malezi bora kwa Watoto wao kuanzia ngazi ya familia pamoja na kuwatimizia mahitaji yao kusudi kuwatengenezea Mazingira rafiki ya kutimiza malengo yao.

Sophia Lucas ambaye ni Katibu wa (UWT) Wilaya ya Butiama amesema kuwa, Kituo cha Nyumba Salama ni muhimu kwani kimekuwa kikiisaidia Serikali kwa kiwango kikubwa kuwapa Hifadhi na kuwaendeleza kimasomo ili wapate fursa ya elimu katika kuwafanya watimize ndoto zao. Huku akiwahimiza wasome kwa bidii. ili kuja kulisaidia Taifa katika nyanja za maendeleo.
Katibu wa UWT Wilaya ya Butiama Sophia Lucas akizungumza katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari kinachohudumia Watoto waliokimbia Ukatili wa Kijinsia walipofika kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika na Kutoa zawadi mbalimbali.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Butiama Anna Jonathan akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara. Ambapo pia UWT walitoa zawadi mbalimbali kwa mabinti hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo Cha Nyumba Salama Kiabakari, Regina Lucas akitoa taarifa ya Kituo hicho,amesema mpaka sasa Kituo hicho kinahudumia Watoto wa kike 51 ambao wapo kituoni hapo kufuatia kukimbia, ukeketaji, ndoa za utotoni na aina nyingine za ukatili.

Ameongeza kuwa, Shirika la (HGWT) linaendelea kufanya kazi kwa karibu sana na Serikali ikiwemo kutoa elimu ya madhara ya Ukatili wa Kijinsia, pamoja na kuwahudumia wahanga wote wa Ukatili wanapofika katika Kituo cha Nyumba Salama sambamba na kuwaendeleza kifani na kielimu ili kutimiza malengo yao.
Sehemu ya mabinti wa Nyumba Salama Kiabakari Butiama Mkoa wa Mara wakiwa wamebeba bango katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Kituo hicho na kuhudhuriwa na UWT Wilaya ya Butiama ambapo pia walipewa zawadi mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news