WABUNGE WAPATIWA SEMINA KUHUSU MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Wabunge wamepatiwa semina kuhusu utekelezaji na umuhimu wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi nchini ili wabunge hao ambao ni wawakilishi wa wananchi waweze kuuelewa mfumo namna unavyotekelezwa na manufaa yake kiuchumi, kijamii na kibiashara.

Semina hiyo imetolewa Juni 28, 2021 Bungeni Mjini Dodoma na wataalam wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakiongozwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula ambapo wasilisho la Mfumo huo na hatua za utekelezaji zilizofikiwa na zinazoenda kufanyika lilitolewa.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akizungumza wakati Wizara hiyo ikitoa semina kwa wabunge kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi pamoja Mada ya mwelekeo wa Shirika la Posta Tanzania iliyofanyika Bungeni Mjini Dodoma. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso.

Akizungumza katika semina hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa nchi inaelekea kwenye uchumi wa kidijitali ambapo mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ndio unaokwenda kurahisisha kufanyika kwa biashara mtandao kwa sababu unawezesha mwananchi kuuza na kununua bidhaa popote alipo kwa njia ya mtandao.

“Wabunge nyie ndio wawakilishi wa wananchi hivyo mkiuelewa mfumo huu maana yake taarifa itakuwa imefika kwa wananchi katika halmashauri takribani 185 na Tanzania nzima itakuwa imeelewa umuhimu wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi,"amesisitiza Mhandisi Kundo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso akizungumza wakati wa semina kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi iliyotolewa kwa wabunge na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bungeni Mkoani Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew.

Aidha, Mhandisi Kundo amesema kuwa ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji na matumizi ya mfumo huo Wizara hiyo imetengeneza programu tumizi ya simu za mkononi (mobile application) ambayo itarahisisha ukusanyaji wa taarifa za makazi, barabara na vituo vinavyotolea huduma za kijamii hivyo kurahisisha utambuzi wa maeneo na kuwezesha mwananchi kufika sehemu anayohitaji kufika kwa kuingia katika programu hiyo ambayo itaonesha njia ya kupita mpaka kufika sehemu husika.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula aliutambulisha Mwongozo wa kurahisisha utekelezaji wa Mfumo huo nchini ambao umepangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 na kuelezea kuwa Wizara iliamua kuandaa mwongozo huo ili kurahisisha na kufanikisha usimikaji wa mfumo huo nchini ambao unahusisha Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula (kushoto) akiteta jambon a Kaimu Postamasta Mkuu Macrise Mbodo wakati Wizara hiyo ikitoa semina kwa wabunge kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi pamoja Mada ya mwelekeo wa Shirika la Posta Tanzania iliyofanyika Bungeni Mjini Dodoma.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (wa kwanza kushoto waliokaa mbele akifuatilia semina iliyotolewa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa wabunge kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi pamoja Mada ya mwelekeo wa Shirika la Posta Tanzania iliyofanyika Bungeni Mjini Dodoma.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo Mhandisi Clarence Ichwekeleza ameuzungumzia Mfumo huo kuwa na manufaa mengi hasa katika kipindi hiki ambacho kutokana na mabadiliko ya teknolojia shughuli nyingi za kiuchumi, kijamii na kibiashara zinafanyika kwa njia ya mtandao hivyo mfumo huo utarahisisha ufikishaji wa huduma mpaka mlangoni ikiwa ni pamoja na huduma zinazotolewa na Shirika la Posta Tanzania.

Aidha, katika semina hiyo wabunge walipitishwa kwa ufupi kuhusu mwenendo wa Shirika la Posta Tanzania ambapo Kaimu Postamasta Mkuu Macrise Mbodo alisema kuwa Shirika hilo limejipanga kuboresha huduma zao kwa kutumia teknolojia ya dijitali ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma ya duka mtandao.
Wabunge wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi pamoja na mwenendo wa Shirika la Posta Tanzania katika semina ambayo Wizara hiyo ilifanya kwa wabunge hao Bungeni Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula (kushoto) wakifurahia jambo na Kaimu Postamasta Mkuu Macrise Mbodo wakati Wizara hiyo ikitoa semina kwa wabunge kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi pamoja Mada ya mwelekeo wa Shirika la Posta Tanzania iliyofanyika Bungeni Mjini Dodoma.

Amesema kuwa katika maonesho ya sabasaba yatakayofanyika mwaka huu Shirika litazindua rasmi huduma ya duka mtandao na kusaini makubaliano na TanTrade ya kuwaingiza na kuwasajili wafanyabiashara wadogowadogo na wa kati kwenye duka mtandao ili waonekane na kutambulika duniani pote kwa bidhaa wanazozalisha.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso amesema kuwa ni vizuri Wizara hiyo kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ndio inayoisimamia NIDA, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuharakisha utekelezaji wa mfumo huo kwa ufanisi na kwa wakati huku akiahidi yeye pamoja na wabunge kuutangaza mfumo huo kwa wananchi pamoja na kulinadi Shirika la Posta Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news