NA GODFREY NNKO, Diramakini Blog
Kila mmoja wetu anatambua kuwa, pamba ni zao la nne linaloingizia Taifa kipato kwa asilimia 99 nchini.
Wadau walioshiriki siku ya wakulima (FIELD DAY) Wilaya ya Maswa katika eneo la Ipililo Juni 25,2021.
Hili ni zao linalolimwa na wakulima wadogo na asilimia 70 mpaka asilimia 80 huuzwa nje ya nchi.
Kwa kutambua thamani ya zao hilo kwa wakulima wa Tanzania na Taifa kwa ujumla, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeendelea kuwa mstari wa mbele kutafiti teknolojia mpya ambazo zitamuwezesha mkulima kupata tija zaidi.
Ndiyo maana, taasisi imekuwa ikiwakutanisha pamoja wadau mbalimbali katika maeneo ya kilimo kwa lengo la kuwapa uelewa wa pamba na namna ya kutumia teknolojia ili mkulima aweze kunufaika katika zao la pamba.
Wadau walioshiriki siku ya wakulima (FIELD DAY) eneo la Ipililo lililopo Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ambao wameoneshwa matokeo ya teknolojia mpya ya upandaji kwa nafasi ndogo kwenye zao la Pamba, wamejifunza mengi.
Mratibu wa zao la Pamba Tanzania, Dkt. Paul Saidia akielezea manufaa ya teknolojia mpya ya upandaji kwa nafasi ndogo kwenye zao la pamba na umuhimu wa kufanya utafiti wa zao la pamba ili kuongeza uzalishaji kwa mkulima.
Hatua hii inakuja, baada ya muda mrefu zao la pamba kutumia teknolojia moja tu katika vipimo vya upandaji wa mbegu.
Teknolojia ambayo watalamu wanaeleza kuwa, imepitwa na wakati na haina matokeo bora.
Teknolojia hiyo ya vipimo iliyokuwa ikitumika katika upandaji wa mbegu ni sentimeta 90 kwa sentimenta 40 (mstari na mstari sentimeta 90 pia mbegu na mbegu sentimeta 40).
Utafiti wa TARI unaonesha kuwa teknologia ya sentimenta 90 kwa 40 imetumika kwa muda mrefu, lakini bado haijamkomboa mkulima nchini.
Ndiyo maana, TARI kupitia teknolojia ambazo wanazifanyia utafiti ili kuleta kwa wakulima zimelenga kuwaomboa wakulima na kupunguza gharama za uzalishaji.
Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu Tanzania, Dkt. E. Lukonge akiongea na wadau walioshiriki siku ya wakulima (FIELD DAY) eneo la Ipililo lililopo Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu. Wadau hao walikuwa wanaonesha matokeo ya teknolojia mpya ya upandaji kwa nafasi ndogo kwenye zao la pamba.
Miongoni mwa teknologia hizo mpya ambazo TARI inazifanyia utafiti ni sentimeta 50 kwa sentimenta 30 (mstari na mstari 50, mbegu na mbegu sentimeta 30) sentimeta 60 kwa 30.
Nyingine ni vipimo vya sentimenta 70 kwa 30 pamoja na sentimeta 80 kwa 30.
Kwa mujibu wa TARI, vipimo hivyo vinaweza kubadilika vikawa sentimenta 50 kwa 16.67,60 kwa 16.67,70 kwa 16.67 pamoja na 80 kwa 16.67.
Lengo lake kubwa ni kuongeza mazao shambani,kwani matumizi ya teknolojia ya zamani 90 kwa 40 imekuwa ikiacha nafasi kubwa na kufanya mkulima kutonufaika kutokana na kupata mazao machache.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Mhe. Aswege Kaminyoge akisisitiza jambo mbele ya wadau kuhusu utumiaji wa teknolojia mpya ya upandaji kwa nafasi ndogo kwenye zao la pamba. (Picha zote na TARI).
TARI inaendelea kusisitiza kuwa,suala la mbolea ni muhimu kwani uchaguzi mzuri wa mbolea hufanya mazao yakuwe kwa ustawi mzuri zaidi.
Pia utumiaji wa mbolea za kisasa ikiwemo urea na mbolea ya kukuzia mmea uweze kuwa na afya nzuri na kuzaa matunda ya kutosha hivyo kuleta matokeo mazuri kwa mkulima.
Hata hivyo, kwa kutumia mbolea kila mche mmoja wa pamba unatakiwa kuwa na vitunda kuanzia 20 na kwenda juu.
Aidha,ukifanya vizuri na kuzingatia kanuni zote mche unaweza kubeba vitunda hadi 40 ambapo inasisitwa kuwa, hata mbolea ya samadi ni sahihi kwa matumizi.
Tags
Habari