NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Rais wa Jamuhuri ya Muugano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itapeleka timu ya wataamu wa sekta ya madini nchini Botswana kujifunza mikakati ya namna ya kuendeleza madini nchini kwa ajili ya biashara duniani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiongoza Ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na Ujumbe wa Botswana uliokuwa ukiongozwa na Rais wao Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akizunguma katika mkutano maalumu na waandishi wa habari uliofanyika Juni 10,2021 Ikulu Dar es salaam wakati wa ziara ya Rais wa Botswana nchini, Mhe. Dkt. Mokgweetsi Keabetswe Masisi, Rais Samia amesema Botswana ni nchi inayofanya vizuri kiuchumi Afrika, ambapo uchumi wake unatokana na kuzalisha kwa wingi madini ya almasi na nyama.
“Botswana ni nchi yenye uchumi mzuri Afrika na inayoongoza duniani kwenye kuuza madini ya Almasi, hivyo mimi na mgeni wangu Mhe. Rais Mokgweetsi Masisi tumekubaliana Tanzaia ipeleke wataamu wa sekta ya madini kule, ili kujifunza uzoefu wao katika eneo hilo na kuweza kufanya vizuri," amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema kwamba katika mazungumzo yake ya faragha na Rais Masisi wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wao wa kirafiki lakini pia wa kibiashara na uwekezaji ambapo uwekezaji wa Botswana nchini umekuwa ukiongezeka kutoka shilingi za kimarekani milioni 731 mwaka 2005 hadi kufikia bilioni 3.5 mwaka 2020.
Kutokana na Botswana kuwekeza kwenye miradi mbalimbali hapa nchini yenye thamani ya Dola za kimarekani shilingi milioni 31, kuna Watanzania wapatao 2,128 ambao wamenufaika na ajira kutoka kwenye miradi hiyo. Rais Samia anatoa wito kwa watanzania wote, kuchangamkia fursa za kibiashara zitakazotokana na uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wa Rais wa Botswana Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi amesema kwamba Tanzania na Botswana zina uhusiano wa kihistoria tangu enzi za kupigania uhuru wa nchi mbalimbali Afrika, hivyo ushiriano baina ya nchi hizi mbili utaleta manufaa kwa pande zote mbili.
“Ushirikiano wetu utaongoza nchi zetu kwa manufaa kila nchi. Tumekubaliana mawaziri wetu wa Mambo ya Nje ndani ya miezi mitatu wakutane na kupanga utaratibu wa kifufua Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ya mwaka 2002 na kufanya mkutano wake wa mwisho mwaka 2009”
Rais Masisi pia alimkaribisha Rais Samia, kwenda kumtembelea nchini Botswana ili kuimarisha uhusiano wao na kupata uzoefu wa mambo mabalimbali, lakini pia alimuahidi kumuunga mkono hasa kwa kuzingatia historia ya nchi zao.