Na Munir Shemweta, WANMM RUVUMA
Watendaji wa Sekta ya Ardhi katika Mkoa wa Ruvuma wametakiwa kushirikiana na kuacha tofauti zao kwenye utendaji kazi ili kuleta ufanisi na tija katika sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa na Afisa Utumishi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Mwajabu Masimba alipozungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Ruvuma wakati wa kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma.
Afisa Utumishi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Mwajabu Masimba akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Ruvuma tarehe 19 Juni 2021 wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma. Kushoto ni Mpima Ardhi wa Wizara Siri Mrisho, wa pili kushoto ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Ruvuma Ildefonce Ndemela na Kulia ni Afisa Mipango Miji wa Wizara Emmile Mwasoge.
Wizara ya Ardhi inaadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza tarehe 16 Juni 2021 na kufikia kilele tarehe 23 juni 2021 kwa kutembelea ofisi zake zilizoko pembezoni ambapo Wizara hiyo inatembelea ofisi zake za mikoa ya Ruvuma na Mtwara.
Amesema, watumishi wa sekta ya ardhi hawatakiwi kutofautiana katika utendaji wowote wa kazi hata kama wako kada tofauti kwa kuwa taofauti yoyote itakayojitokeza haitaleta tija kwenye sekta ya ardhi.
Kwa mujibu wa Bi. Masimba, kufanya kazi maeneo ya pembezo si kama wamewatenga watumishi wa maeneo hayo bali ni sehemu ya majukumu na ndiyo maana Wizara ya Ardhi iliamua kupeleka timu ya maafisa wake ili kujua na kuzipatia ufumbuzi changamoto zao.
‘’Tushirikiane kila moja kwa kazi yake na mkumbuke muda mwingi tunautumia ofisini hivyo ushirikiano mtakaoufanya kwenye utendaji kazi na kuondoa tofauti utaifanya wizara kusonga mbele kwa kuwa taswira nzuri ya ofisi inajengwa na watumishi,’’amesema Masimba.
Naye Afisa Mipango Miji kutoka Idara ya Maendeleo ya Mkazi Wizara ya Ardhi Bi. Emmile Mwasoge aliwatia moyo watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Ruvuma kuwa wasikate tamaa kutokana na changamoto zilizopo na kuwataka kuwa wavumilivu.
‘’Wapo wananchi wengi wanaotaka ajira hivyo ninyi mliobahatika kupata kazi mvumilie na mchape kazi mambo mazuri yatakuja tu,’’ amesema Bi.Mwasoge.
Mmoja wa Watumishi wa sekta ya Ardhi katika mkoa wa Ruvuma akiwasilisha changamoto za kiutendaji kwenye eneo lake mbele ya Timu ya Maafisa wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo tarehe 19 Juni 2021 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 16 Juni 2021 ambapo Wizara ya Ardhi katika kuadhimisha wiki hiyo iliamua kutembelea ofisi zake zilizoko pembezoni.
Afisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi Idara ya Maendeleo ya Makazi Emmile Mwasoge akichukue changamoto za baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Ruvuma tarehe 19 Juni 2021 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 16 Juni 2021 ambapo Wizara ya Ardhi katika kuadhimisha wiki hiyo iliamua kutembelea ofisi zake zilizoko pembezoni.
Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Ruvuma Ildefonce Ndemela akisisitiza jambo wakati wa kusikiliza changamoto za watumishi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Ruvuma tarehe 19 Juni 2021 ikiwa ni Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 16 Juni 2021 na kufikia kilele Juni 23, 2021 ambapo Wizara ya Ardhi katika kuadhimisha wiki hiyo inatembelea ofisi zake zilizoko pembezoni. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Ruvuma Ildefonce Ndemela aliwakumbusha watumishi wa sekta ya ardhi katika mkoa wake kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wakati changamoto zao zikifanyiwa kazi.
Awali Watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Ruvuma walieleza changamoto za kiutendaji na binafsi zinazowakabili katika maeneo yao ambapo baadhi yake ni upungufu wa watumishi na vifaa vya kutendea kazi kama vile magari.
Watumishi ambao Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Ardhi ilisikiliza chanagmoto zao ni kutoka Ofisi za Ardhi mkoa wa Ruvuma zinahusisha Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa, Halmashauri za Mbinga Mji, Mbinga DC, Tunduru, Manispaa ya Songea, Nyasa, Songea DC, Madaba pamoja na Halmashauri ya Namtumbo.
Tags
Habari