WAZIRI MKUU MAJALIWA: SIJARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA EPZA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) wilayani Ubungo ambapo amesema hajaridhishwa na utendajikazi wa mamlaka hiyo, hivyo ameagiza yafanyike mabadiliko makubwa kuhakikisha lengo ya uanzishwaji wake linafikiwa.

“…Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda (Dotto James) waondoe hapa Mkuu wa Kitengo cha Sheria Sara Mwaipopo na Meneja Uwezeshaji Grace Lemunge kwa sababu wanafanyakazi kwa mazoea na urasimu mkubwa. Hapa hatuhitaji urasimu, tunataka wawekezaji.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua jengo la uwekezaji, wakati alipotembelea Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje jijini Dar es Salaam (EPZA), Juni 18, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi wa kampuni ya Somani Agro Exports Ltd, Dkt. Alykhan Somani(katikati) kuhusu nafaka ambayo ipo tayari kusafirishwa kwenda nje ya nchi, wakati alipotembelea kampuni hiyo iliyopo ndani ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) jijini Dar es Salaam, Juni 18, 2021. Kushoto ni Afisa Uhusiano Lilian Kimei. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Juni 18, 2021 wakati akizungumza na watumishi baada ya kutembelea eneo la EPZA lililopo wilayani Ubungo, Dar es Salaam. Amesema hajaridhishwa na viwango vya uwekezaji kwa sababu ya urasimu uliokuwepo EPZA na amewataka watumishi wabadilike.

“Kampuni 18 zilizoomba kuwekeza katika eneo hili zimekataliwa kwa sababu ya urasimu uliopo hapa EPZA. Mwaka 2020 kampuni 18 ziliomba leseni kwa ajili ya uwekezaji katika eneo hili lakini kati yake kampuni tano tu ndio zilipewa leseni, wengi walionekana hawana sifa….vikwazo vingi ni urasimu tu.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia nguo zinazozalishwa na kiwanda cha kutengeneza nguo cha Tooku, kilichopo ndani ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) jijini Dar es Salaam, Juni 18, 2021. Kiwanda hicho kinazalisha nguo milioni sita kwa mwaka, kikiuza zaidi kwenye soko la nchini Marekani. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia swichi zilizong’olewa na muwekezaji katika jengo la uwekezaji wakati alipotembelea Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) jijini Dar es Salaam, Juni 18, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema kuna baadhi ya kampuni ziliomba eneo kwa ajili ya uwekezaji tangu mwaka 2018, ambapo majibu wameyapata mwaka huu tena wamekataliwa. Serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza katika eneo hilo, watumishi wanatakiwa wafanye kazi kwa bidii ili kutimiza lengo la uwekezaji huo.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameagiza kutafutwa kwa watu wote waliohusika na ung’oaji wa vifaa likiwemo jenereta moja kubwa pamoja, AC na swichi za umeme katika moja ya jengo la mamlaka hiyo. Ametoa agizo hilo baada ya kuingia ndani ya jengo hilo na kushuhudia vitu hivyo vikiwa vimeng’olewa.

“Hatua kali zichukuliwe kwa aliyeng’oa vitu katika jengo lile. Lazima kazi ifanyike kwa kuzingatia weledi, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona kazi zikiwa zimeshamiri hapa na eneo hili livutie wawekezaji. Tunataka mambo yaende vizuri ili nchi izidi kupata maendeleo.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia nguo zinazozalishwa na kiwanda cha kutengeneza nguo cha Tooku, kilichopo ndani ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) jijini Dar es Salaam, Juni 18, 2021. Kiwanda hicho kinazalisha nguo milioni sita kwa mwaka, kikiuza Zaidi kwenye soko la nchini Marekani (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia usukaji wa transfoma wakati alipotembelea karakana ya kiwanda cha kuzalisha bidhaa za nishati cha AFRICAB iliyopo Kiwalani jijini Dar es Salaam, Juni 18, 2021. Kulia ni Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Mauzo wa kampuni ya AFRICAB David Tarimo (kushoto) kuhusu uzalishaji wa nyaya za umeme wakati alipotembelea karakana ya kiwanda hicho iliyopo kurasini jijini Dar es Salaam, Juni 18, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Mauzo wa kampuni ya kuzalisha bidhaa za nishati ya AFRICAB, David Tarimo (kushoto) kuhusu transfoma iliyotengenezwa na kampuni hiyo jijini Dar es Salaam, Juni 18, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Hivi jenereta hapa linaibiwaje na linapitaje katika geti?…si rahisi mtu atoke Mbagala aje aibe hapa mmeiba nyie wenyewe. Mkurugenzi fuatilia kujua nani anaiba vifaa kwa sababu hakuna mtu anayeweza kuingia katika eneo hili bila ya kufuata taratibu.”

Maeneo mengine yaliyotembelewa na Waziri Mkuu katika eneo hilo ni pamoja na kiwanda cha kushona suruaji za jeans cha Tooku ambacho soko kubwa la bidhaa zake liko nchini Marekani. Kiwanda kingine alichokitembelea ni kiwanda cha nafaka cha Somani.

Pia, Waziri Mkuu ametembelea viwanda vya Africab ambavyo ni kiwanda cha kutengeneza transfoma kilichopo Kiwalani pamoja na kiwanda cha kutengeneza nyaya za umeme kilichopo Kurasini. Waziri Mkuu ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji mkubwa ulioufanya kwenye sekta ya nishati nchini.

Waziri Mkuu amesema uzalishaji huo umekuwa chachu ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijiji kwani kabla ya kampuni hiyo kuanza uzalishaji wa bidhaa nchini Serikali ilikuwa inatumia gharama kubwa kuagiza nje ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news