Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuwa na kasumba ya kufanya mazoezi kila siku kwa ajili ya kulinda afya zao jambo ambalo litasaidia kuepukana na magonjwa nyemelezi ambayo ushambulia miili yao, anaripoti DOREEN ALOYCE (Diramakini Blog).
Waziri Mkuu ameyasema hayo kwenye Bonanza la michezo lililoandaliwa na Benki ya CRDB na kufanyija katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma ambalo liliwashirikisha wabunge,watumishi wa Serikali na wananchi.
Aidha, amesema Bonanza hilo lina lengo la kuhamasisha mshikamano kwa Watanzania na ushiriki katika shughuli za maendeleo huku akiipongeza Benki ya CRDB kuandaa Bonanza hilo lililopewa jina la "CRDB Benki pamoja Bonanza"
Pia amesema bonanza hilo linatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kuwaleta Watanzania pamoja na kushirikiana katika shughuli za kijamii na uchumi wa Taifa letu.
“Wengi tunajua faida ya michezo hususani kutulinda na magonjwa ila tumeshuhudia Mheshimiwa Rais katika hotuba zake alituasa tukitaka kwenda haraka twende peke yetu, lakini tukitaka kwenda mbali twenda pamoja niwapongeze Benki ya CRDB kwa kuonyesha mfano wa kutuleta pamoja Bunge, Wizara pamoja na Wananchi wote kupitia CRDB Benki Pamoja Bonanza,” amesema Waziri Mkuu
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka taasisi nyengine za umma na binafsi kuiga mfano wa Benki ya CRDB kwa kuandaa mabonanza kama hilo ilikuendelea kujenga utamaduni wa michezo na mshikamano miongoni mwa Watanzania Jambo ambalo litazidi kuimarisha afya za watu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema lengo kuu la kuandaa bonanza hilo ni kuisogeza benki hiyo karibu na Serikali, Bunge na Wizara, ili kupata nafasi ya kusikiliza mahitaji yaliyopo na kujua namna gani benki hiyo inaweza shiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya nchi.
"Miaka ya nyuma tulikuwa tukifanya bonanza hili na Bunge, mwaka huu tumeshirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kushirikisha Wizara zote Malengo yetu mwakani ni kuhusisha muhimili mwengine wa Serikali kwa maana ya Mahakama,” ameongezea Nsekela.
Nae, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dkt. Tulia Ackson ameiomba Benki ya CRDB kuendeleza utamaduni huo ambao wamekuwa nao kila mwaka Wa kushirikiana na Bunge katika kuhamasisha michezo na kujenga mahusiano.
“Tunawapongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa bonanza hili kwa mara nyingine tena, hii ni njia nzuri sana ya kujenga mahusiano huku tukiimarisha afya zetu,” amesema Tulia.
Akikabidhi kombe na medali kwa mshindi wa jumla Benki ya CRDB, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amewapongeza washindi katika bonanza hilo na kuwashukuru watumishi wote wa Serikali, Bunge, Benki ya CRDB na wananchi waliojitokeza kushiriki katika bonanza hilo.
Hata hivyo, katika Bonanza hilo, timu ya Benki ya CRDB iliibuka mshindi katika mpira wa miguu, timu ya Bunge iliibuka mshindi katika mpira wa kikapu na katika mpira wa pete timu ya Watumishi wa Wizara iliibuka mshindi.
Mbali na hayo kulikuwa na michezo mingine ya burudani ikiwamo kuvuta Kamba, kukimbia na magunia, kufukuza kuku, mchezo wa bao, karata, draft, pamoja na pool table.
Tags
Habari