Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog
WAZIRI wa Mambo ya Ndani George Simbachawene, amewaahidi wananchi wa Kitongoji cha Chihikwi Kata ya Mbalawala jijini Dodoma kuhakikisha anamaliza mgogoro wa ardhi kati yao na Jeshi la Magereza uliodumu zaidi ya miaka nane na kupelekea mvutano ambao unarudisha nyuma maendeleo.
Wananchi wa Kitongoji cha Chihikwi Kata ya Mbalawala wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene (hayupo pichani ) alipofika kutatua changamoto ya ardhi baina yao na Jeshi la Magereza Msalato jijini Dodoma.
Inadaiwa kuwa, mgogoro huo ni kutokana na wananchi kuvamia ardhi ya Gereza Msalato ambapo wengi wamejenga makazi yao huku wengine wakifanya shughuli zao za kilimo na ufugaji.
Kauli hiyo imekuja mara baada ya Waziri Simbachawene kufika katika kitongoji hicho kwa lengo la kumaliza mgogoro huo wa kaya 86 waliovamia kwa kuwaeleza kugawiwa hekari 20 ambapo kila mmoja atapata robo heka.
Akizungumza na wananchi hao katika Viwanja vya Kitongoji hicho,Waziri Simbachawene amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kupunguza migogoro ya ardhi nchini na amemtuma kuumaliza mgogoro baina yao na Jeshi la Magereza Msalato kwa kuwagawia robo heka kila familia ili waweze kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za kulijenga Taifa.
Amesema, baada ya kupatiwa viwanja hivyo kila mwananchi hatua itakayofuatwa ni urasimishwaji kufanyika na mamlaka husika ya ardhi.
Aidha, maamuzi hayo ya Waziri hayakuungwa mkono na baadhi ya wananchi baada kutokuridhishwa na makubaliano hayo ya awali, wakidai kupewa fidia na kwamba Serikali kuangalie upya suala la ugawaji ardhi kwani robo heka ni ndogo na tayari kuna watoto ambao wamefikisha umri wa miaka 18 hawana sehemu za kuishi na pia hakuna sehemu za kujenga taasisi mbalimbali za huduma ya jamii.
"Tunashukuru Serikali kwa kutaka kumaliza mgogoro huu, lakini tunaomba kuongezewa hekari kwani robo heka ni ndogo sana haijitoshelezi tayari tuna watoto wakubwa wenye miaka 18 tunaomba mliangalie kwa jicho la pili,"amesema Peter Anton.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mbalawala, Charles Ngambi amesema wakati muhafaka wa wananchi kuridhia na Serikali kumaliza mgogoro huo ambao umerudisha maendeleo nyuma kwani hakuna waliojenga nyumba nzuri na hakuna huduma za kijamii.
Amesema, kumalizika kwa mgogoro huo utasaidia watu kufanya maendeleo huku Serikali ikileta huduma za kijamii hususani hospitali, elimu, barabara, umeme na maji.
"Niwaombe wananchi wangu tuwe wasikivu na kutoa ushirikiano kwa Serikali yetu lengo ni kuondoa mgogoro kati yetu na majirani zetu Magereza ili tuishi kwa amani na upendo,"amesema Ngambi.
"Niwaondoe wasiwasi nimewasikiliza nitarudi tena mapema sana kumaliza huu mgogoro, lakini mtambue kuwa ardhi ni mali ya umma, Serikali inaangalia maslahi ya Taifa haitamuonea mtu na kuhusu fidia huwa inalipa kama ardhi imeendelezwa sasa naomba mjitafakari kuhusu hilo, haiwezekani mtu ana nyumba ina thamani ya elfu sabini halafu anadai fidia kila mmoja atapewa haki yake," amesema Simbachawene.
Awali Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Suleiman Mzee amesema, jeshi mwaka 1986 lilikuwa na ardhi ukubwa wa hekari elfu 13 lakini kadri wananchi wanavyovamia mpaka sasa zimebaki hekari 7,315.
Amesema, licha ya hayo Jeshi na kamati za usuluhishi lilikaa na kukubaliana kutolewa kwa hekari 20 kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa Kitongoji hicho.
Mgogoro huo umedumu kwa miaka nane na wananchi hao na Jeshi la Magereza, ambapo wananchi wanasema eneo hilo ni haki yao na mpaka wa Magereza upo mbali nao, na wapo hapo tangu enzi za wazazi wao ambao walishafariki.
Huku nao Jeshi la Magereza wanasema wananchi hao wamevamia eneo hilo jeshi na wana nyaraka ambazo zimethibitishwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA).
Tags
Habari