NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu leo Juni 24, 2021 ametoa ufafanuzi ufuatao kufuatia mijadala inayoendelea kuhusu Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
"Nafurahi kupokea maoni na ushauri kutoka kwa waheshimiwa madiwani, watumishi wa halmashauri na wananchi kuhusu suala hili. Nimefurahi kujua kuwa wote tunakubaliana kuwa lipo tatizo la kusimamia utendaji katika halmashauri zetu za wilaya, miji, manispaa na majiji.
"Aidha tumebaini kuwa Sekretarieti za mikoa hazina meno ya kusimamia nidhamu za Watumishi walioko katika mamlaka za Serikali za Mitaa.
"Ili wananchi waweze kupata huduma bora na maendeleo endelevu na kwa haraka ni lazima tulitatue tatizo hili. Nimewaomba Ofisi ya Rais Utumishi kushirikiana na wizara yangu kulifanyia kazi suala hili,"amesema.
"Waheshimiwa Madiwani wenzangu haya ni mawazo yetu. Najua watumishi wenu wamefurahia sana hili. Tutaangalia na upande wa pili. Maoni yenu ni muhimu sana. Tutayazingatia.
"Niwatoe hofu waheshimiwa madiwani wenzangu kuwa tutafanya uamuzi wa pamoja juu ya namna bora ya kuimarisha usimamizi wa utendaji katika halmashauri zetu. Pia ninawaahidi kuwa tutafanya mafunzo elekezi kwa waheshimiwa madiwani wote nchini ili kuongeza uelewa kuhusu usimamizi bora wa utendaji na rasilimali za umma katika halmashauri zetu. Lengo letu ni kuona changamoto za maendeleo ya wananchi zinatatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi,"amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Tags
Habari