Yanga SC yabadili matokeo dakika ya 90, wengine wachechemea

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Wanajangwani Yanga SC wamewasogelea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC baada ya ushindi wa mabao matatu waliyoyapata leo.
Ushindi huo wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Mwandui FC wameupata katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Yanga SC wanatinga nafasi ya pili wakiwa na alama 67 baada ya mechi 31huku nafasi ya kwanza ikiwa chini ya watani wao Simba SC.

Ni katika kabumbu safi ambalo kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu zote mbili kufungana bao 1-1.

Hofu ilizuka baada ya Mwadui FC kutangulia kufunga dakika ya saba kupitia kwa Aniceth Revocatus.

Aidha, Yanga SC walisawazisha dakika ya 21 kupitia kwa Bakari Mwamnyeto, hivyo kuwapa nguvu mpya.

Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi ya kawaida na dakika ya 55 Mwadui FC walifanya mabadiliko kwa kumtoa Makyada Makolo na nafasi yake kuchukuliwa na Denis Richard.

Aidha, Tuisila Kisinda wa Yanga dakika ya 59 aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Zawadi Mauya aliyekuwa akicheza eneo la kiungo mkabaji sambamba na Mukoko Tunombe.

Ndani ya dakika ya 65, Aniceth alipachika bao la pili kwa timu yake ya Mwandui FC kwa kupiga shuti kali nje ya boksi la Yanga.

Wanajangwani walifanya mabadiliko mengine dakika ya 68 kwa kumtoa Fiston Abdul Razack aliyeonekana kukosa nafasi nyingi za wazi na kuingia Yacouba Sogne.

Pia dakika ya 75 Mwadui FC walifanya mabadiliko kwa kumtoa Richars aliyeingia kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Amri Msenda.

Mabadiliko ambayo yalifuatiwa na ya Yanga SC dakika ya 80 wakimtoa Said Ntibazonkiza na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri Junior.

Aidha, dakika ya 90, Yacouba aliisawazishia Yanga SC baada ya kulishambulia lango la Yanga mfululizo kwa dakika zisizopungua tano.

Hatimaye, Junior alifunga hesabu kwa Yanga SC kwa kuwapa bao la tatu na la ushindi katika mechi hiyo, hivyo kujikusanyia alama tatu.

Wakati huo huo bao pekee la Abdulmajid Mangalo dakika ya 45 limewapa wenyeji, Biashara United ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Ni katika mtanange uliopigwa katika dimba la Karume mjini Musoma mkoani Mara.

Matokeo hayo yanaifanya Biashara United kufikisha alama 49 baada ya kucheza mechi 32, hivyo kuwa nafasi ya nne.

Wakati huo huo, Kagera Sugar wamelazimishwa sare ya bila kufungana na Ihefu SC ya Mbarali, Mbeya Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kagera Sugar inafikisha alama 37 za mechi 32 sasa na kupanda kwa nafasi moja tu hadi ya 11, ikiwazidi wastani wa mabao Mtibwa Sugar ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi.

Hata hivyo, Ihefu FC inafikisha alama 35 za mechi 32 na inabaki nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news