Zanzibar yaipongeza Ujerumani kwa kuiunga mkono

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Serikali ya Ujerumani kwa utayari wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo iliyopangwa na Serikali ya Awamu ya Nane.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bi Regine Hess.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Balozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Nchini Tanzania Mhe. Regine Hess, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Hess kuwa azma ya Serikali ya Ujerumani ya kuendelea kuisaida Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuyafikia malengo yaliyowekwa.Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia, inathamini sana mashirikiano yaliopo kati yake na Serikali ya Ujerumani na hatua yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya ambayo itandelea kuletea manufaa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema kuwa azma ya Serikali ya Ujerumani ya kusaidia uendelezaji wa mradi wa maji safi na salama pamoja na mitaro ya maji taka katika eneo la Mji Mkongwe itasaidia katika kuuweka mji huo katika hadhi yake inayotajika sambamba na kuwapelekea wananchi kupata huduma hizo ipasavyo.Alifahamisha kuwa Serikali ya Ujerumani kwa muda mrefu imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya afya hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuzisaidia hospitali ya Abdalla Mzee Pemba na Hospitali ya Kijeshi ya Bububu.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba mbali ya Zanzibar kusaidiwa katika kuendeleza miradi katika sekta ya afya ni vyema ikasaidiwa katika uendelezaji miundombinu na mifumo ya afya pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu ili kuwe na tija endelevu ya misaada inayotolewa.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Ujerumaini kuja kuekeza Zanzibar kwa kutumia fursa zilizopo hasa kupitia sera yake ya uchumi wa buluu kwani ndani yake mna mambo mengi ya kuekeza yakiwemo utalii, uvuvi, mafuta na gesi pamoja na kuzitumia rasilimali nyengine za bahari.

Katika sula zima la uwekezaji, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane, tayari imeshaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na iko tayari kuwapokea.Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Serikali ya Ujerumaini kuiunga mkono Zanzibar katika mapambano dhidi ya maradhi ya COVID 19 ambayo yameikumba dunia nzima.

Mapema, Balozi wa Ujerumani nchini Bi Regine Hess, kwa upande wake alisema kuwa Zanzibar na Ujerumani zina historia kubwa ya mashirikiano hivyo Ujerumani itayaendeleza mashirikiano hayo kwa kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Nane katika kuendelza miradi iliyojiwekea.Balozi Hess alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali yake iko tayari kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo huduma za maji safi na salama pamoja na mitaro ya maji taka katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Aliongeza kuwa Mji Mkongwe wa Zanzibar una mashirikiano mazuri na Serikali ya Ujerumani kwani miradi kadhaa ya miundombinu yake imetekelezwa na nchi hiyo.Aidha, Balozi Hess alisema kuwa kwa upande wa Sekta ya afya Serikali ya Ujerumari iko tayari kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo hapa nchini.Balozi Hess pia, alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa na Ubalozi huo katika kuitangaza Zanzibar kiutalii ikiwa ni pamoja na kuwaleta wawekezaji kutoka Ujerumani kuja kuekeza hapa Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Balozi Hess alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba kutokana na Zanzibar kujaaliwa kuwa na viungo ambavyo ni miongoni mwa vivutio vya kitalii, hatua za makusudi atazichukua katika kutafuta soko nchi Ujerumani.Sambamba na hayo, Balozi Hess alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za makusudi alizozichukua za kuhakikisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa inamarika na kuleta manufaa kwa nchi na wananachi wa Zanzibar.

Pia, Balozi Hess alieleza kwamba hatua hizo alizozichukua Rais Dk. Mwinyi ni za kuungwa mkono kutokana na azma yake ya kuendeleza amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar sanjari na kuieletea Zanzibar maendeleo endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news