Na Mwandishi Maalum, Dar
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Bw. Sylvester Mwakitalu amefanya ziara ya ukaguzi katika Magereza ya Keko na Gereza Kuu Ukonga yaliyopo mkoani Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya magereza hayo, kuzugumza na mahabusu pamoja na wafungwa na kuahidi kushirikiana na vyombo vingine kutatua changamoto zinapelekea kuwepo kwa msongamano ndani ya magereza hayo.
Mkuu wa Gereza la Mahabusu Segerea, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, SSP Daniel Mwakyoma akiwaongoza viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka, DPP Sylvester Mwakitalu kuelekea Gereza la Mahabusu wanaume.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo aliyoongozana na baadhi ya watendaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mashtaka,DPP Mwakitalu amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea hali halisi ya magereza, kuwasikiliza mahabusu na wafungwa ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili mahabusu na wafungwa kufuatia kesi mbalimbali zilizopo mahakamani.Zinazohusiana soma, DPP Mwakitalu ateta na watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
“Ujio wangu hapa ni kwa ajili ya kujionea hali halisi ya msongamano pamoja na kusikiliza kero za mahabasu, wafungwa na magereza kwa ujumla ili niweze kufanyia kazi maeneo yale yanayohusu ofisi yangu,"amesema DPP Mwakitalu.
Mkurugenzi wa Mashtaka, DPP Sylvester Mwakitalu akisalimiana na baadhi ya maafisa wa magereza katika gereza la Mahabusu Segerea mkoani Dar es salaam wakati wa ziara yake.
Mkurugenzi Mwakitalu amesema, Magereza mengi nchini yanakabiliwa na msongamano mkubwa wa wafungwa na mahabusu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa hali ya uhalifu nchini.
Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu amewataka watanzania kuacha kujihusisha na uhalifu hali ambayo inachangia kuongezeka kwa msongamano magerezani huku akiahidi kufanya kazi kwa nguvu na bidii ili mashauri yaweze kusikilizwa kwa haraka na wakati.
Mkurugenzi wa Mashtaka, DPP Sylvester Mwakitalu (Kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Gereza la Mahabusu wanawake Segerea Mrakibu wa Magereza Iyunge Saganda (wa pili kutoka kushoto) wakati wa ziara ya kutembelea na kusikiliza changamoto za Mahabusu.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Mashtaka ametembelea na kujionea uzalishaji mkubwa wa bidhaa (samani) zinazotengenezwa na wafungwa katika gereza kuu Ukonga.
Ziara hiyo ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini imelenga katika kusikiliza, kupokea malalamiko na changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya mashtaka ili ofisi yake iweze kuyatafutia ufumbuzi ili kupunguza changamoto na msongamano magerezani.
Tags
Habari