NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mwanamke mmoja, Zawadi Sayi Abdallah (pichani) mkazi wa Kidinda Halmashauri ya Mji wa Bariadi, amewalalamikia wahudumu wa afya katika hospitali ya halmashauri hiyo (Somanda) kumpatia mtoto mmoja badala ya watoto wawili (mapacha).Tukio hilo la kustahajabisha, linadaiwa kutokea Mei 23, 2021 baada ya Zawadi kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua huku akiwa ameambatana na mama yake mzazi, Joyce Lujiga ambaye alikuwa amemsindikiza.
Zawadi pamoja na mama yake (Joyce) walisema wakiwa nyumbani kwao wameieleza DIRAMAKINI Blog kuwa, walishangaa pia kuona wanatakiwa kugharamikia vifaa tiba na dawa ambavyo vilihitajika kwenye zoezi la upasuaji.
Kwa mujibu wa Zawadi, siku hiyo baada ya kufika hospitalini hapo majira ya mchana alipimwa na madaktari (majina tunayahifadhi) na kumwambia kuwa ana mapacha hivyo anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
“Baada ya majibu hayo ya vipimo, walimweleza mama yangu (Joyce) kuwa anatakiwa kusaini fomu za kwenda kufanyiwa upasuaji, naye mama akawasiliana na Baba yangu na Mme wangu wakaruhusu ndipo nikapelekwa chumba cha upasuaji,” amesema Zawadi.
Mama yake Zawadi (Joyce) anasema kuwa, baada ya zoezi la upasuaji kwenda vyema huku mtoto wake Zawadi akiwa hajitambui, alishangaa kuona analetewa mtoto mmoja wa kiume badala ya mapacha kama ambavyo waliambiwa mwanzo.
“Kwa kuwa mtoto wangu Zawadi alikuwa hajitambui kutokana na zoezi la upasuaji na dawa za usingizi, niliona wananiletea mtoto mmoja, nikashangaa, nikawauliza mtoto mwingine yuko wapi?...
“Daktari huyo huyo aliyetupima mwanzo, akasema mtoto ni mmoja huyo tu…hakuna mwingine bali alikuwa mkubwa kilo nne, nikabaki nashangaa na Zawadi baada ya fahamu kurejea akashangaa anapewa mtoto mmoja,” alisema Joyce.
Baada ya majibu hayo Zawadi na mama yake Joyce akiwa na mtoto wake mmoja wa kiume waliruhusiwa kwenda nyumbani na kuwaeleza wanafamilia na kuamua kukaa kimya kwani walifikiri majibu ya madaktari yalikuwa sahihi.
“Baada ya wiki mbili kupita, nilirudi hospitalini hapo kwa ajili ya kusafishwa kidonda, ndipo nilipokutana na mkunga mmoja jina lake silijui baada ya kuniona nikiwa nimekaa kwenye benchi nasubiria huduma huku nikiwa nimebeba mtoto wangu...
“Yule mkunga (nesi) aliniuliza mbona nimebeba mtoto mmoja, mwingine yuko wapi, mimi nilimkatalia nikamwambia labda unanifananisha, akasema wewe si unaitwa Zawadi…nikamwambia ndiyo, akasema yeye alikuwepo wakati wa upasuaji nilijifungua watoto wawili, nikabaki nashangaa kasha akaondoka,” anaeleza Zawadi.
Mwanamke huyo anasema kuwa baada ya kuambiwa hivyo alikwenda moja kwa moja kwa mama yake kumweleza alichokutana nacho, na familia nzima kuanza kushangaa na kurejea majibu ya daktari kuwa yalikuwa uongo na majibu ya vipimo yalikuwa kweli.
Mama yake Zawadi (Joyce) anasema kuwa baada ya kuletewa taarifa mpya na Zawadi, aliamua kwenda hospitali kueleza taarifa hizo kama zina ukweli na apate majibu mtoto yuko wapi.
“Nilifika kwa viongozi wa hospitali nilichokutana nacho ni majibu ya kejeli tu, wahudumu wote ambao walihusika kwenye upasuaji waliitwa, lakini walianza kunishambulia kwa maneno ya kejeli…nikawauliza mtoto yuko wapi hawakunijibu nikaamua kuondoka,” amesema Joyce.
Anasema kuwa, baada ya kutopata majibu aliamua kurejea nyumbani na kukaa kimya huku wakitafakari wapi wanaweza kwenda kwa ajili ya kupata haki yao.
Gharama wakati wa kujifungua
Mbali na lalamiko hilo Mama yake Zawadi (Joyce) anasema kuwa, kabla ya zoezi la upasuaji alipatiwa orodha ya vifaa na Daktari vinavyohitajika wakati wa upasuaji na kuelezwa anatakiwa kwenda nje ya hospitali kwenye maduka ya dawa muhimu kununua vifaa hivyo.
“Orodha ilikuwa ndefu sana, nilipokea karatasi hiyo nikaenda kwenye duka la hospitali wakanitajia gharama za vifaa vyote zikawa kubwa zaidi ya 150,000 ndipo nikatoka nje ya hospitali nikanunua vifaa hivyo kwa sh. 130,000,” amesema Joyce.
Akionyesha stakabadhi yenye orodha ya vifaa hivyo pamoja na dawa, ilionekana kuwa na vifaa mbalimbali ikiwemo maji tiba (drip) pamoja na plastiki za kuvaa mikononi (gloves).
Uongozi wa Hospitali
Alipotafutwa Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Said Mlowosha kujibu tuhuma hizo, alikiri ofisi yake kupata malalamiko ya Mwanamke huyo huku akibainisha kuwa ni kweli alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua.
Dkt. Mlowosha ameeleza kuwa katika uchunguzi wa awali ambao wameufanya kukagua taarifa zake kwenye mafaili kuanzia alipopimwa hadi chumba cha upasuaji zilizonyesha kuwa hakuna sehemu ambayo iliandikwa kuwa ana mapacha.
“Taarifa zote kwenye mafaili yake zinaonyesha alikuwa na mtoto mmoja ambaye alikuwa mkubwa uzito wa kilogramu 3.3, lakini tunaendelea na uchunguzi zaidi kubaini ukweli juu ya majibu na hicho kilichotokea,” alisema Dkt. Mlowosha.
Aidha, aliongeza kuwa uchunguzi wa kina ambao unaendelea ni kubaini mhuguzi aliyemwambia Zawadi wakati aliporejea hospitalini hapa kwa ajili kusafishwa kidonda, ili kuweza kujua kama ni kweli au hapana.
Mbali na hayo Dkt .Mlowosha alizungumzia suala la mteja huyo kutakiwa kununua vifaa vyote vya upasuaji, ambapo alisema sera inaeleza kuwa huduma kwa mama wajawazito ni bure hivyo nalo wanalifanyia uchunguzi.
Tags
Habari