Na Mathew Kwembe, Arusha
Timu ya JKT Mbweni ya Dar es salaam imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Netiboli Ligi daraja la kwanza mwaka huu baada ya kuwafunga Mabingwa wa Kombe la Muungano la Netiboli mwaka 2019 TAMISEMI QUEENS kwa magoli 40-39 katika mchezo mkali na wa kusisimua uliofanyika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Mfungaji bora wa Mashindano ya Netiboli Ligi daraja la Kwanza Lilian Jovin wa TAMISEMI QUEENS akifunga mojawapo ya magoli katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo ambapo TAMISEMI QUEENS walifungwa na Mbweni JKT magoli 39-40.
TAMISEMI QUEENS wakiongozwa na nahodha wa timu hiyo Sophia Komba na wafungaji wake hatari Lilian Jovin na Aziza Itonye waliutawala mchezo huo mwanzo hadi mwisho wa mchezo na kuwafunika kabisa wachezaji Frida Zablon na Doritha Mbunda wa JKT Mbweni ambao iliwabidi kutumia nguvu kuwakaba wachezaji wa TAMISEMI QUEENS.
Hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika TAMISEMI QUEENS walikuwa mbele kwa magoli 10-8.
Katika robo ya pili na ya tatu TAMISEMI QUEENS waliongoza kwa magoli 19 -18 na robo ya tatu waliongoza kwa magoli 29-28.
Washindi wa pili wa Ligi ya Netiboli TAMISEMI QUEENS wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa mchezo kati yake na Mbeni JKT.
Hata hivyo Mchezo huo ulianza na dosari tangu dakika ya kwanza ya mchezo baada ya refarii namba moja Masumbuko Matata kutoka Mwanza na refarii namba mbili Enock Akyoo wa Mtwara kuamua waziwazi kuibeba timu ya JKT Mbweni.
Katika mchezo huo uliokuwa umetawaliwa na ubabe na kukamiana kwingi Mwamuzi Matata aliwaachia wachezaji wa Mbweni JKT kucheza faulo mara kwa mara hasa golikipa wa Mbweni JKT Joyce Kaila alikuwa akiwafanyia faulo za wazi wafungaji wa TAMISEMI QUEENS Lilian Jovin (GS) na Aziza Itonye (GA) jinsi alivyotaka bila mwamuzi huyo kumchukulia hatua zozote.
Nyota wa mchezo wa leo alikuwa ni mchezaji Aziza Itonye (GA) wa TAMISEMI QUEENS ambaye mara kwa mara alikuwa akiipasua ngome ya JKT Mbweni na kulazimika kufunga magoli akiwa mbali kwa kuhofia kufanyiwa faulo na wachezaji wa JKT.
Nahodha wa Mbweni JKT Joyce Kaila akinyanyua juu kombe la klabu bingwa Netiboli baada ya mchezo wao wa mwisho dhidi ya TAMISEMI QUEENS.
Mchezo huo ambao ulishuhudiwa na Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni sanaa na Michezo Mhe. Paulina Gekul ambaye aliwataka CHANETA kuhakikisha katika mashindano yajayo ihakikishe inateua waamuzi bora na wenye weledi wa kuchezesha mashindano ya ligi daraja la kwanza nchini.
Kauli ya Naibu Waziri iliungwa mkono na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt Athumani Kihamia ambaye baada ya kumalizika kwa mchezo huo alionyesha dhahiri kukerwa na Kitendo cha Mwamuzi Masumbuko Matata wa Mwanza kushindwa kuumudu mchezo huo.
“Huyu refa aliyechezesha leo kutoka Mwanza mimi siwezi kumung’unya maneno hakuchezesha kihalali na tunaweza kusema ameyatia aibu mashindano haya,” amesema Dkt Kihamia.
Mchezaji Bora wa Mashindano ya Ligi ya Netiboli Meryciana Kizenga kutoka TAMISEMI QUEENS akipokea zawadi yake kutoka kwa Naibu Waziri Mhe.Paulinen Gekul.
Dkt.Kihamia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Michezo mkoa wa Arusha amesema anatarajia tukio kama hilo hataliona mwakani katika mashindano ya Ligi daraja la kwanza na badala yake aliwataka CHANETA kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanaamuliwa na marefa walio huru na uwezo.
“Kwa refa kuchezesha vile ama hana uwezo au kachukua rushwa ama timu mojawapo inamhusu, kwa hiyo mwakani tutahakikisha mambo ya namna hii hayatokei katika mkoa wetu,” alisema Dkt Kihamia.
Mchezaji Bora wa kati wa Mashindano hayo Sophia Komba wa TAMISEMI QUEENS akipokea zawadi yake kutoka kwa Naibu Waziri Mhe.Paulinen Gekul.
Katika mashindano hayo Timu ya TAMISEMI QUEENS ilifanikiwa kutoa mfungaji bora wa mashindano hayo Lilian Jovin, Mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP) Meryciana Kizenga na Mchezaji bora wa kati wa mashindano hayo Sophia Komba.
Jumla ya timu 13 zilishiriki mashindano hayo yaliyoanza julai 19 na kuhusisha timu tisa za wanawake na timu nne za wanaume, ambapo washindi watatu wa kwanza wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Netiboli Afrika Mashariki na timu sita za mwanzo zitashiriki katika kombe la Netiboli Zanzibar katika mashindano yatakayofanyika baadaye mwaka huu.
Tags
Michezo