MAKAMBA: KUCHIMBA MADINI VYANZO VYA MAJI NI KUUA KIZAZI CHA SASA NA KIJACHO

Na Yusuph Mussa, Bumbuli

MBUNGE wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba amewataka viongozi wa Serikali za vijiji, kata hadi wilaya kushirikiana kutunza mazingira, kwani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu kuchimba madini kwenye vyanzo vya maji katika Kata ya Vuga, kunaathiri kizazi cha sasa na kile kijacho.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (kushoto) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kihitu mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye zahanati ya kijiji hicho. (Picha na Yusuph Mussa).
Aliyasema hayo Julai 30, 2021 wakati anazungumza kwenye Kikao cha Kamati ya Maendeleo (WDC) Kata ya Vuga kwa kusema uharibifu unaofanywa kwenye chanzo cha maji Nkindoi na maeneo mengine, ni vitu ambavyo havikubaliki, na suala hilo atalifikisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Calist Lazaro.

"Rasilimali za nchi hii ikiwemo misitu na vyanzo vya maji sio mali yetu, bali tumerithishwa na mababu zetu kama dhamana tu, ili kizazi kijacho kiweze kukuta mali zao. Sasa itashangaza kama mzee (Bakari) Kijemkuu (Mwenyekiti wa CCM Kata ya Vuga), unataka kufa na kila kitu kilichopo sasa. Mimi niombe viongozi wa vijiji na kata, shirikianeni na wananchi kuona mnalinda urithi huu wa watoto na vitukuu vyetu kwa vizazi vijavyo. Mnapoharibu vyanzo vya maji mnajimaliza ninyi wenyewe.

"Madini unachukua wewe na mke wako, mnakwenda kujenga nyumba na kununua bodaboda, lakini sisi unatuachia uharibifu wa mazingira kwa miaka yote. Afadhali basi ungechukua hayo madini halafu tukagawana wote tujue moja. Na nataka niseme, kama kuna viongozi wapo humu wanashirikiana na hao wachimbaji waache. Nawahakikishia suala hili nitalifikisha kwa Mkuu wa Wilaya ili kuweza kuchukua hatua stahiki katika kulinda mazingira na urithi wetu" alisema Makamba.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (wa pili kulia) akikagua maabara ya Shule ya Sekondari Kiviricha iliyopo Kata ya Usambara. Ni baada ya kufanya ziara Julai 30, 2021. (Picha na Yusuph Mussa

Diwani wa Kata ya Vuga Jumaa Dhahsbu alisema baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi za kata hiyo pamoja na wananchi, wapo hatarini kukumbwa na magonjwa kutokana na maji ya bomba wanayokunywa kuchanganyika na kemikali zinazotoka kwenye machimbo ya madini, sababu machimbo hayo yapo katikati ya vyanzo vya maji.

"Kwa zaidi ya miaka 10 sasa, wachimbaji hao wamekuwa wakiondolewa kwa nyakati tofauti, lakini baada ya muda wanarudi. Na kwa sasa wanachimba madini hayo usiku. Na wanafunzi wa shule ambao wanaathirika na tatizo hili ni shule za msingi Bazo, Vuga na Emau. Pia kuna Shule ya Sekondari Vuga na Chuo cha Biblia Vuga" alisema Dhahabu.

Lakini pia kuna misikiti mitatu, makanisa mawili, na wananchi wanaoishi vijiji vya Bazo na Kishewa. Na mradi mwingine wa maji utakapokamilika, pia wananchi wa Kijiji cha Baghai ikiwemo Shule ya Seminari ya KKKT na Shule ya Msingi Baghai, makanisa mawili, na misikiti miwili wataathirika.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (wa tatu kushoto) akikagua ujenzi wa chumba cha darasa Shule ya Sekondari Kiviricha, Kata ya Usambara. (Picha na Yusuph Mussa).

Akizungumza wakati anaweka jiwe la msingi Zahanati ya Kihitu katika Kata ya Vuga, Makamba alisema wananchi wameonesha jitihada kubwa katika kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo ambao umefikia karibu asilimia 80, pamoja na fedha za Mfuko wa Jimbo, Serikali na wadau wengine, wananchi wamechangia kwa kiasi kikubwa.

Makamba alisema kwa hatua iliyofikia, sasa ni kazi yake kuhakikisha anapeleka wahudumu wa afya pamoja na dawa. Na hayo ndiyo malengo ya Serikali kuona wananchi wanapata huduma za afya karibu.

Akizungumza na mwandishi wa habari mara baada ya zoezi la kuweka jiwe la msingi Zahanati ya Kihitu kumalizika, Diwani, Dhahabu alisema ujenzi wa zahanati hiyo ulianza Machi 2017, na wananchi wamechangia nguvu kazi na michango jumla ya sh. milioni 18 na Mfuko wa Jimbo sh. milioni 2.4.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga January Makamba (katikati) akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa wananchi wa Kata ya Usambara. Ni baada ya kufika Shule ya Sekondari Kiviricha. (Picha na Yusuph Mussa).

Dhahabu alisema akitumia fedha yake ya mfukoni, Makamba alichangia bati 200 zenye thamani ya sh. milioni tano, sh. 870,000 kwa ajili ya kukusanya mawe ya ujenzi, na jana Julai 30, 2021 ametoa sh. 500,000 kwa ajili kuweka nguzo mbili ili umeme ufike kwenye zahanati hiyo.

Naye Katibu wa Mbunge, Hozza Mandia, alisema katika Kata ya Usambara, Makamba kwa fedha zake za mfukoni, alitoa mifuko 70 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kwandoghoi, mifuko 30 Zahanati ya kwampunda, fedha taslimu sh 300,000 za uchimbaji wa barabara inayochimbwa na wananchi kutoka Kijiji cha Kiviricha hadi Kwamzuza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news