Marekani yaipatia Tanzania dozi milioni 1.06 za chanjo ya Corona

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Leo Julai 24,2021 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea awamu ya kwanza ya dozi za chanjo ya covid-19 aina ya Johnson & Johnson 1,058,400 kutoka serikali ya Marekani na kueleza kuwa imefuata miongozo yote na kujiridhisha na usalama wake kwa matumizi ya binadamu.

Chanjo hiyo itaanza kutolewa baada ya kukamilika kwa taratibu za ndani za serikali huku makundi maalumu wakiwemo wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 50 yakiwa kipaumbele.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Doroth Gwajima, katika hafla ya kupokea msaada wa chanjo hizo iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Dkt.Gwajima amesema, kuingia kwa chanjo hiyo, kumezingatia miongozo yote iliyowekwa na serikali na kwamba huo ni mwanzo wa chanjo nyingi zinazotarajiwa kuingia nchini.

Amesema, serikali kupitia tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imejiridhisha na kuruhusu kupokelewa kwa chanjo hiyo.

"Chanjo hii ni salama na imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Kamati iliyoundwa na Rais Samia na serikali tutaendelea kujirithisha kwa kila chanjo itakayoingia nchini," amesema.

Ameeleza kuwa, chanjo hiyo itatolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya na baadhi ya vituo vitakavyoanzishwa ili kusogeza huduma karibu kwa wananchi.

Pia amebainisha baada ya kukamilika kwa utaratibu ndani ya serikali, wataanza kutoa kwa wananchi kwa kuzingatia muongozo, ambapo makundi maalumu ndiyo yatakayopewa kipaumbele.“Tumepanga baada ya kukamilika kwa utaratibu wa ndani wa serikali tutaanza kuitoa bure na kwa hiari na hii tutazingatia muongozo wa kipaumbele kwa makundi maalumu ambayo ni wahudumu wa afya, wazee wa zaidi ya miaka 50 na wenye magonjwa nyemelezi,”amesema.

Aidha, amesema ujio wa chanjo hiyo isiwe sababu ya wananchi kuacha kuendelea kuchukua afua nyingine za kujikinga na janga hilo.

“Chanjo zina historia ya kupingwa na baadaye zinakimbiliwa, mara nyingi zimekuwa zikikabiliana na magonjwa kabla hata ya dawa kupatikana, mtakumbuka namna chanjo zilimaliza magonjwa kama Surua, Pepopunda na mengineyo,” amefafanua.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberatha Mulamula amesema, wizara yake itaendelea kushirikiana na wabia kupata chanjo za kukabiliana na janga hilo na kwamba Tanzania haiwezi kuishi kama kujitenga.

Amebainisha kuwa, chanjo ndiyo njia sahihi ya kujenga kinga kwa binadamu na kwamba hatua iliyofikiwa sasa ni matunda ya jitihada za serikali.

“Mimi nimesimama hapa pia muhanga wa janga hili, familia yangu inasumbuliwa na Covid-19 kwa hiyo ugonjwa huu upo, muhimu tujikinge,” amesema.

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini, Dkt. Donald Wright amesema, msaada huo wa dozi milioni moja ya chanjo ya Covid-19 aina ya Johnson & Johnson ni sehemu ya jitihada za kimataifa za kukabiliana na janga hilo.

Amesema, chanjo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa serikali ya Marekani ya kutoa dozi milioni 25 kwa nchi za Afrika kati ya dozi milioni 80 zilizoahidiwa kwa Bara hilo.

Dkt.Wright amesema, uratibu wa shughuli hiyo unahusisha Umoja wa Afrika (AU) na Kituo cha Kudhibiti Maradhi (Africa CDC).

"Tunachangia chanjo hizi ili kuokoa maisha na kuiongoza dunia katika kulitokomeza janga hilo, pia mchango wetu huu ni kielelezo cha uimara wa ushirikiano wetu wa miaka 60 na dhamira yetu ya dhati kwa Tanzania," amesema Balozi huyo.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani, (WHO), Dkt. Tigest Katsela amesema, kwa sasa Dunia ina visa zaidi ya milioni 191, huku Afrika ikiwa na visa milioni 4.5 na vifo 108,000.Amesema, kutokana na athari hizo ni budi kujenga nguvu za pamoja katika kukabiliana janga hilo ili kuokoa uchumi wa mataifa mbalimbali duniani.

Marekani ina furaha kutangaza kuipatia Tanzania zaidi ya dozi milioni moja za chanjo dhidi ya COVID-19, msaada uliotolewa kupitia mpango wa usambazaji chanjo kimataifa wa #COVAX kwa uratibu wa Umoja wa Afrika. Marekani inachangia chanjo hizi ili kuokoa maisha na kuiongoza dunia katika kulitokomeza janga hili. Aidha, kuchangia kwetu chanjo hizi ni kielelezo cha uimara wa ubia wetu wa miaka 60 na dhamira yetu ya dhati kwa Tanzania.

Tutaendelea kuchangia chanjo salama na zenye ufanisi kwa wingi kadri itakavyowezekana, kwa watu wengi duniani kadri itakavyowezekana na kwa haraka kwa kadri itakavyowezekana hadi pale janga la COVID-19 litakapokuwa limetokomezwa kabisa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news