Mbunge Shekilindi awahakikishia Ubiri umeme unakuja

Na Yusuph Mussa, Lushoto

MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi amewahakikishia wananchi wa Kata ya Ubiri kuwa sasa watapata umeme na maji, kwani huduma hizo zimekuwa duni kwa muda mrefu mpaka kuwafanya wananchi kukata tamaa.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi 'Bosnia' (kulia) Julai 27, 2021 alifika Kitongoji cha Mkuzi- Wanilo, Kijiji cha Migambo, Kata ya Migambo kukagua nguzo za umeme kama zimefika maeneo yote yaliyokusudiwa kabla ya kuanza kusimikwa ili wananchi wapate umeme. (Picha na Yusuph Mussa).

Aliyasema hayo Julai 26, 2021 alipofika Kijiji cha Ubiri, Kata ya Ubiri kwenye mkutano wa hadhara, ambapo baadhi ya wananchi waliouliza maswali, huku wakiwa wamekata tamaa kuona huduma ya umeme, maji na barabara za vijiji bado ni kero kwao.

"Tumechoka kuona kila siku wafanyakazi wa TANESCO wanakuja kwenye vijiji vyetu wanapima na kuweka vigongo. Walikuja mara ya kwanza wakaweka vigongo. Lakini walirudi mara ya pili wakaweka vigongo. Na sasa hivi wameweka vigongo mara ya nne. Tumeachoka kuona vigongo sasa tunataka tuone nguzo za umeme" alisema Ramadhan Mbilu.

Juma Makono alisema chanzo cha maji kutoka Irente kimekuwa ni hadthi kila siku, kwani ni miaka mingi wameelezwa watapata maji kutoka huko, lakini hadi sasa hawajapata maji hayo, hivyo wanaomba kama kuna chanzo kingine, basi wataamini watapata maji, lakini sio kutoka Irente.

Jamal Sabuni alisema barabara za kata hiyo ni mbovu, hivyo kumuomba Mbunge kuwataka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuweza kutengeneza barabara hizo kwa kiwango cha changarawe, kwani wakati wa mvua wanawake wajawazito wanashindwa kufika kwenye vituo vya huduma ya afya. Lakini hata wanafunzi kwenye shule za msingi na sekondari ni wahanga wa tatizo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi 'Bosnia' (katikati) Julai 27, 2021 alifika Kitongoji cha Mkuzi- Wanilo, Kijiji cha Migambo, Kata ya Migambo kukagua nguzo za umeme kama zimefika maeneo yote yaliyokusudiwa kabla ya kuanza kusimikwa ili wananchi wapate umeme. (Picha na Yusuph Mussa).

Shekilindi alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya kweli ya kuwafikishia huduma zote wananchi wake, na kuongeza kuwa Serikali ilianzisha Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mwaka 2019 kwa minajili ya kuwapatia wananchi maji kwa uhakika. Lakini pia, Serikali ilianzisha TARURA kwa malengo hayo hayo ya kuhakikisha barabara za vijijini zinatengenezwa na kupitika mwaka mzima.

"Nataka niwahakikishie vyanzo vyote vya maji ikiwemo Irente vitaleta maji kwenye Kata ya Ubiri. Kilichokuwa kinatatiza maji yasifike sio vyanzo vya maji bali ni pesa. Hivyo baada ya Serikali kuona tatizo la maji ni kubwa hapa nchini, ilianzisha Wakala wa Maji RUWASA ili kuona wananchi wanapata maji kwa uhakika zaidi, kwani Serikali imewekeza fedha nyingi kwa wakala huyo.

"Lakini pia kuna Wakala wa Barabara TARURA. Hawa wanahakikisha barabara za mijini na vijijini zinapitika wakati wote. Ninyi wote ni mashahidi mmenisikia nikirindima bungeni kuhakikisha barabara ya Dochi- Ngulwi- Mombo (kilomita 16) inafanyiwa kazi, na ikibidi iwekwe lami sababu ni barabara muhimu kwetu. Pia kuna barabara ya Mlalo- Ngwelo- Mlola- Makanya- Milingano hadi Mashewa ya kilomita 70. Hii ni muhimu kwa wakulima na wafanyabiashara, nayo itatengenezwa" alisema Shekilindi.

Shekilindi alisema Serikali imelipendelea Jimbo la Lushoto, kwani limelipatia sh. bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Sh. bilioni 3.5 ni kwa ajili ya barabara ya Mlalo- Ngwelo- Mlola- Makanya- Milingano hadi Mashewa kwa kiwango cha changarawe, huku sh. bilioni moja kwa ajili ya kuweka lami kutoka Hospitali ya Wilaya ya Lushoto hadi Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Na sh. milioni 500 ni matengenezo ya maeneo korofi na barabara za vijijini.

Lakini pia kuna mradi mkubwa wa maji wa kata 13 ikiwemo Ubiri ambao utagharimu zaidi ya sh. bilioni 20. Mradi huu utakuwa mkombozi kwa wananchi wengi wa Jimbo la Lushoto. Kuhusu umeme, alisema kwa sasa nguzo 20 zinawekwa kila kijiji, na baada ya hapo kupitia Kamati za Maendeleo za Kata (WDC) wataandika mihutasari ya kuomba umeme kwenye vitongoji.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi 'Bosnia' akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ubiri, Kata ya Ubiri (hawapo pichani) Julai 26, 2021, ikiwa ni ziara ya kukagua miradi ya maendeleo, ambapo Julai 27, 2021 alifika Kitongoji cha Mkuzi- Wanilo, Kijiji cha Migambo, Kata ya Migambo kukagua nguzo za umeme kama zimefika maeneo yote yaliyokusudiwa kabla ya kuanza kusimikwa ili wananchi wapate umeme. (Picha na Yusuph Mussa)

Katika mkutano huo, kupitia Mfuko wa Jimbo, Shekilindi alitoa mifuko ya saruji 10 na nondo tano kwa ajili ya Zahanati ya Kijiji cha Miegeo. Pia alitoa mifuko ya saruji 10 na nondo tano Zahanati ya Kizara vyote vikiwa na thamani ya sh. 530,000. Pia ametoa sh. milioni tatu ili kukamilisha vyumba vinne vya Shule ya Msingi Handei- Ubiri (Shikizi) ili ikamilike na kupata usajili.

Shekilindi, pamoja na kutoa elimu juu ya ugonjwa wa corona (UVIKO 19) kwenye mikutano hiyo, pia amekuwa akitoa dawa ya corona, ambayo yeye ndiyo mgunduzi na mtengenezaji, kwa wazee 20 kila kata anayokwenda. Ameshatoa dawa hiyo kwa kata tano za Kilole, Makanya, Mlola, Ngwelo na Ubiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news