Mike Sonko kuwataja viongozi wenye Ukimwi ambao wamekuwa wakiambukiza Wanawake na wenzao kwa makusudi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Gavana mstaafu wa Kaunti ya Nairobi nchini Kenya, Mike Mubuvi Sonko ambaye pia ni mjasiriamali mashuhuri nchini humo ametangaza kuvujisha siri za viongozi wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) ambao wamekuwa na tabia za kuwalaghai Wanawake na kufanya nao ngono bila kutumia kinga.
Hatua hiyo imeonekana kumsononesha Mheshimiwa Sonko, kwa kuwa kufanya hivyo si tu kwamba wanawaambukiza virusi bali wanawafanyia ukatili.

"Haki ya Mungu viongozi wengine ni wajinga sana na wanastahili kuchomwa. Yani unajijua uko na ukimwi but instead of using rubber ama mpira kazi yako ni kuambukiza viongozi wenzako na innocent women plus kuwapea mimba. Pepoo wewe. Ngoja tu utaskia very soon,"ameandika Sonko katika ukuta wake wa kijamii.
Sonko ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi wenye ujasiri na wanaojali zaidi wananchi wa daraja la chini, wakati wa uongozi wake alijizolea umaarufu mkubwa kwa kuwa mstari wa mbele kusikiliza mtu mmoja mmoja au makundi na kuyapa usaidizi pale panapostahili.

Mwishoni mwa mwaka jana ndipo Bunge la Seneti nchini Kenya lilipiga kura kumuondoa Mike Mubuvi Sonko kama gavana wa Nairobi.

Kura ambayo ilihitimisha miaka mitatu yake ya utumishi huku wananchi wengi wakilalama kwa uamuzi huo.

Mheshimiwa Sonko alituhumiwa kwa ukiukaji wa katiba, matumizi mabaya ya madaraka, utovu wa nidhamu na uhalifu chini ya sheria.

Maseneta 27 walipiga kura kuunga mkono kuondolewa ofisini kwa Sonko kwa kudumisha mashtaka yote manne yaliyowasilishwa na Bunge la Kaunti ya Nairobi, ambalo lilipiga kura ya kutokuwa na imani naye Desemba 3, mwaka jana.

Bw. Sonko alichaguliwa kuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi mwaka 2017, kupitia chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta.

Aidha, viongozi hao wawili walitofautiana, hivyo kufikia hatua ya Rais Kenyatta kushinikiza mageuzi yaliyochangia majukumu makuu ya Kaunti ya Nairobi kuhamishiwa Serikali ya Kitaifa.

Rais Kenyatta pia alimteua jenerali wa kijeshi kuendesha shughuli za kaunti, hali iliyomfanya Bw. Sonko kuwa gavana asiye na mamlaka.

Mike Sonko alijipatia umaarufu kutokana na mtindo wake usio wa kawaida alipokuwa mbunge wa eneo la Makadara, Nairobi.

Mike Sonko anafahamika kwa kuvalia vito, mikufu na bangili za thamani.

Alipokuwa mbunge, alikuwa akiandamana kutetea wanyonge na wachuuzi walipokuwa wanatimuliwa kutoka maeneo yao ya kazi na serikali ya jiji.

Pia anakumbukwa kwa kuongoza waandamanaji Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) The Hague, Uholanzi kulalamikia kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta ambayo baadaye ilisitishwa.

Alipokuwa Seneta, alianzisha kundi kwa jina Sonko Rescue Team ambalo lilikuwa likitoa huduma kama vile maji, matibabu na misaada wakati wa mazishi.

Wakati mmoja alipoitwa kusaidia familia zilizokuwa zimeathiriwa na bomoa bomoa jijini mwaka 2014, alimpigia simu Rais Kenyatta na kumuweka kwenye kipaza sauti. Rais alitoa agizo ubomoaji usitishwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news