Mwakamo awakunjulia makucha wanaotoa lugha chafu kuhusu chanjo, tozo

Na Rotary Haule,Kibaha

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo (CCM),amekunjua makucha yake mbele ya wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kibaha kwa kuwatolea uvivu baadhi ya viongozi na wananchi wanaotoa lugha za chafu za kumkashifu Rais Samia Suluhu Hassan juu ya chanjo ya Uviko -19 na tozo ya miamala ya simu kwa kuwataka wafunge midomo yao.

Aidha,Mwakamo amesema kuwa Rais Samia amepokea kijiti cha Urais katika mazingira magumu, lakini amekuwa Rais wa mfano kwa kuwa anafanya mambo ambayo yanalenga kuiwezesha jamii na wananchi kuishi kwa furaha na amani, lakini inashangaza kuona watu wanaanza kuleta chokochoko zisizo na tija kwa Taifa.

Mwakamo ametoa kauli hiyo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha kilichofanyika Julai 28, mwaka huu katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha uliopo Kisabi katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Mlandizi .

Katika kikao hicho,Mwakamo amesema kuwa, anawashangaa baadhi ya viongozi na wabunge wa CCM akiwemo mbunge wa Jimbo la Kawe kutoa lugha za kumkatisha tama Rais Samia huku akisema jambo hilo sio sahihi.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo (CCM).

Amesema kuwa,Taifa la Tanzania ni sawa na mataifa mengine na nchi yetu inakwenda kwa mujibu wa sera na maadili na Rais Samia anafanyakazi kubwa ya kutetea wananchi wake.

Alisema ,Rais Samia amefanya utafiti wa kutosha kupitia wataalamu wake na ameona ipo haja ya kuleta chanjo nchini kwakuwa kuna watu wanamahitaji na chanjo hiyo lakini amekwenda mbali zaidi kwakusema chanjo hiyo ni hiari lakini bado watu wanaleta chokochoko.

Mwakamo,aliwaomba wajumbe wa kikao hicho wawe makini na wasikubali kuona Rais Samia anaonewa kwa kusemwa maneno yasiyostahili na badala yake wasimame mstari wa mbele kukemea maneno yanayosemwa na watu hovyo.

" WanaCCM tusimame imara tusikubali Rais wetu aonewe kwakusemwa maneno ya hovyo na wote tunajua Rais ameruhusu kuletwa kwa chanjo kwa faida ya Watanzania ambao wanahitaji ya chanjo kulingana na maeneo na shughuli wanazofanya,"alisema Mwakamo.

Kuhusu tozo katika miamala ya simu Mwakamo alisema, ipo lugha gongana kutoka kwa wananchi, lakini ukweli ni kwamba kilio hicho kimesikika na Serikali inakwenda kulifanyia kazi.

Alisema, wabunge walipitisha tozo hizo kwa ajili ya faida kwa Taifa kwa kuwa fedha zitakazopatikana zitakwenda kusaidia katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara, elimu,afya na huduma nyingine za kijamii.

Mwakamo aliwaasa wajumbe hao kuacha kutoa mwanya kwa watu kuongea bila utaratibu huku akisema wasubiri Serikali itakuja na majibu muafaka ya namna ya kurekebisha jamabo hilo.

"Kuhusu tozo wabunge wamesikia kilio hicho, lakini Rais Samia amesikia kilio cha wananchi wake kwahiyo wajumbe tulieni ili tuiache Serikali ifanyekazi yake ili itoe majibu sahihi maana Rais wetu ni msikivu,"alisema Mwakamo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri,alisema kuwa wajumbe wanapaswa kutoka na azimio la kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya tangu aingie madarakani na pongezi hizo sio kwa wanaCCM tu bali hata kwa wapinzani kwakuwa wapo wapinzani walionufaika na Rais.

Msafiri alisema suala la chanjo ni hiari na hakuna mtu wa kulazimishwa huku akitaka watu waache kutumia siasa katika chanjo kwakuwa miongozo ipo wazi huku akiwataka wanaCCM kuelimisha watu kuhusu chanjo.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Hawa Mchafu akiwa katika kikao hicho alisema kuwa bajeti ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia iliyoanza kutekelezwa Julai mwaka huu ni bajeti bora zaidi.

Hata hivyo, Mchafu alisema kuwa,kupitia bajeti hiyo kila jimbo litapata kiasi cha sh.bilioni 1.5 fedha ambazo zitakwenda kutumika katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara mijini na vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news