Naibu Waziri Dkt.Mabula:Sijaridhishwa na utoaji wa hatimiliki za ardhi Katavi

Na Munir Shemweta, KATAVI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ameonesha kutoridhishwa na utoaji hatimiliki za ardhi kwenye mkoa wa Katavi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikabidhi Mpango Kabambe wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kwa Mkurugenzi wa Manispaa Michael Nzyungu (kushoto) na Meya wa Manispaa hiyo Haidari Subi wakati wa uzinduzi uliofanyika wilayani Mpanda mkoani Katavi jana.

Hali hiyo inafuatia kuelezwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Katavi Geofrey Martine Kamugisha wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake tarehe 20 Julai 2021 kuwa, kasi ya uandaaji hatimiliki imeongezeka ambapo hadi kufikia Juni mwaka huu jumla ya hati 520 ziliandaliwa na kusajiliwa ukilinganisha na hati 2,637 zilizoandaliwa katika mkoa wa Katavi tangu nchi ipate uhuru.

Dkt. Mabula ambaye yuko katika ziara ya siku moja mkoa wa Katavi alisema, kasi ya umilikishaji ardhi katika mkoa wa Katavi bado ni ndogo na kubainisha kuwa idadi hiyo ya hatimiliki za ardhi zilizoandaliwa na kusajiliwa inaweza kutolewa na halmshauri moja.

“Yaani mkoa uwe na hati 520 ambazo ni hati zinazoweza kutolewa na halmashauri, inaonesha hakuna juhudi zozote za kumuwezesha mwanachi,” alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akionesha Mpango Kabambe wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi mara baada ya kuuzindua jana.

Akitolea mfano wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kuwa imetoa jumla ya hatimiliki 270 ikiwa ni wastani wa halmashauri hiyo kutoa hati moja kwa siku na kueleza kuwa, hali hiyo inaonesha halmashauri hiyo haijaona umuhimu wa kuwawezesha wananchi.

” Wakati tunasena ardhi ni mtaji itunze ikutunze lakini hapa hatujaona umuhimu hivyo niombe katika hili mkoa usimamie hasa kwa wakurugenzi wa halmashauri,” alisema Naibu Waziri wa Ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikata utepe kuzindua ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda jana mkoani Katavi uliojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Akigeukia suala la ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi, Dkt Mabula amesikitishwa na mkoa wa Katavi kukusanya mapato ya ardhi kwa asilimia 18.4 ya malengo kufikia juni 2021 na kuomba kuwemo usimamizi katika suala hilo ambapo alisisitiza kuwa, zisipofanyika juhudi katika suala hilo itaidhoofisha serikali kuendesha shughuli zake.

“Kama mkoa unakusanya asilimia 18.4 ya malengo hapo kuna kazi ya kufanya na naomba taarifa ya mapato ya kodi ya ardhi itolewe kwenye vikao vya madiwani vya kila robo mwaka na wananchi pia wanahitaji kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi” alisema Dkt Mabula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news