Naibu Waziri Mabula apiga marufuku wanaoshitakiana Mabaraza ya Ardhi kugharamia usafiri

Na Munir Shemweta, SONGWE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amepiga marufuku wananchi wanaoshitakiana kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya kugharamia usafiri wa kwenda uwandani wakati wa kusikiliza mashauri ya ardhi.

Akizungumza wakati wa kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya, mkoa wa Songwe, Dkt, Mabula alisema, asingependa kuona wananchi wanaoshitakiana katika kesi ya ardhi mmoja wao atoe fadhila ya usafiri wa kwenda uwandani.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kushoto) akioneshwa picha ya anga ya Mji wa Tunduma inayoelezea program ya kupanga, kupima na kumilikisha vipande ardhi na Afisa Mipango Miji wa mkoa wa Songwe Joseph Towo wakati wa uzinduzi Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya katika mkoa wa Songwe jana. Aliyevaa miwani ni Mkuu wa wilaya ya Songwe Simon Simalenga.

"Tusingependa wale wanaoshitakiana mmoja wao atoe fadhila ya usafiri maana baada ya hapo mara nyingi wazee wa Baraza wanashawishika na kuona anayetoa usafiri kuwa amekuwa ni msamamaria mwema kwa hiyo wanamlipa fadhila hata kama hana haki ya kupata ushindi,"alisema Naibu Waziri Mabula.

Aliwataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi kuandaa ratiba za mashauri ya Ardhi kwenye maeneo yao na kuzipeleka kwa wakuu wa wilaya aliowaeleza kuwa watashirikiana na wakurugenzi wa halmashauri kuangalia ratiba na kutoa usafiri kwa wazee wa mabarza ili kwenda uwandani wakati wa mashauri.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimpatia Kompyuta Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma mkoa wa Songwe, James Francis kwa ajili ya kusaidia utendaji kazi wa shughuli za ardhi katika halmashauri hiyo wakati wa uzinduzi Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya katika mkoa wa Songwe.

Naye Kamishna wa Ardhi Nchini Methew Nhonge alisema pamoja na kuwa sheria ya ardhi imeanisha utaratibu mzuri wa kisheria katika kushughulikia migogoro ya ardhi lakini halmashauri na ofisi za ardhi za mikoa zinao wajibu mkubwa wa kuhakikisha migogoro ya ardhi kabla haijaenda mahakamani inatatuliwa kwa njia ya kiutawala.

"Bahati nzuri katika wizara tumeweka utaratibu kwa nchi nzima kuhakikisha kwamba viongozi wa ardhi wa mkoa pamoja na halmashauri kupitia watendaji wa sekta wanaenda kwenye ngazi za halmashauri na mitaa kutoa elimu na kushughulikia migogoro ya wananchi kiutawala,’’ alisema Nhonge.

Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya nchini Stela Tullo aliushurukuru uongozi wa mkoa wa Songwe kwa kusaidia kupata jengo la Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya na kueleza kwamba, uanzishwaji baraza hilo utasaidia kuondoa usumbufu waliokuwa wakiupata wananchi wa Songwe kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Baraza mkoani Mbeya.

"Ninawasihi wananchi wa Songwe kulitumia vizuri baraza la ardhi la mkoa wa Songwe kupata huduma, ile migogoro ya ardhi iliyoshindwa kusuluhishana nyumbani hata katika ngazi ya familia na mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata basi serikali imewasogezea huduma kwenye baraza la ardhi na nyumba la wilaya mkoa wa Songwe,’’ alisema Stela Tullo.

Kabla ya uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, mkoa wa Songwe, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alizindua Baraza kama hilo wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ambapo aliagiza mashauri ya ardhi yasikilizwe na kuisha katika kipindi kisichozidi miaka miwili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news