Na James K. Mwanamyoto-Pwani
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma nchini kulipa deni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kutumia weledi wao kujenga uchumi wa taifa.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Mhe. Ndejembi amesema kuwa Mhe. Rais alipoingia madarakani, alitoa maelekezo kwa Waajiri wote kuzingatia maslahi ya watumishi wa umma hususani suala la upandishwaji wa madaraja jambo ambalo hivi sasa limetekelezwa na linaendelea kutekelezwa na waajiri wote kikamilifu ikiwa ni pamoja na kulipa stahili za watumishi kwa wakati.
Amesema waajiri wote nchini wametekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, hivyo Watumishi wa Umma hawana budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kwani hakuna haki isiyokuwa na wajibu.

“Ni muda mrefu tumekuwa tukililia haki ya kupandishwa madaraja na kupewa stahili nyingine, Rais wetu ametusikia kwani wote waliostahili kupanda madaraja, wamepanda na wenye madai ya stahili zao mbalimbali wamepatiwa, hivyo hili ni deni na ili kulilipa deni hili tunapaswa kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kujali maslahi ya Watumishi wa Umma kwasababu watumishi ndio injini ya Serikali, hivyo wanalazimika kuendelea kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Aidha, Mhe. Ndejembi amezungumzia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika zoezi la upandishwaji wa madaraja kwa Watumishi wa Umma kutokana na baadhi yao kukosa sifa kwa kutojaza Fomu ya Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).


“Changamoto ya upandishwaji madaraja kwa baadhi ya Watumishi ni kupuuza ujazaji wa OPRAS, hawajazi kwa wakati na wanajaza kwasababu wanaona ni kigezo tu cha upandaji wa madaraja.” Mhe. Ndejembi amefanua.
Ili kuongeza ufanisi kiutendaji, Mhe. Ndejembi amewahimiza Watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha lengo la Serikali la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Mhe. Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma kushiriki katika kutoa elimu kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanaonufaika na Mradi wa kutoa ajira za muda.


Amesema suala la usimamizi wa walengwa wa TASAF ni la watumishi wote, hivyo ni vema watumishi wenye utalaam katika fani mbalimbali wakatoa elimu ya kuwawezesha walengwa kutimiza malengo yao badala ya kuwaachia Waratibu wa TASAF pekee.
Aidha, amewataka walengwa wa TASAF kutumia vizuri ruzuku wanayoipata kujikwamua katika lindi la umaskini ili hapo baadae waache kutegemea ruzuku ya TASAF.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema kilio kikubwa cha Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kilikuwa ni suala la upandishwaji wa madaraja jambo ambalo limetekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.


“Mhe. Naibu Waziri tunashukuru sana kwa kututembelea, changamoto kubwa iliyokuwa ikitusumbua ni upandishwaji wa madaraja, suala ambalo limeshafanyiwa kazi, tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuliona hili na kulitekeleza.” Mhe. Ridhiwan ameongeza.
Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi katika halmashauri hizo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma, kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF, ikiwa ni pamoja na kujiridhisha na utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais ya upandishwaji wa madaraja kwa Watumishi wa Umma nchini.