Papa Francis afanyiwa operesheni kubwa kwenye utumbo mpana

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.– Vatican

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 majira ya jioni alilazwa kwenye Hospitali ya Gemelli iliyoko mjini Roma kwa ajili ya kufanyia operesheni kubwa kwenye utumbo mpana.Operesheni hii imeongozwa na Prof. Sergio Alfieri huku akisaidiwa na Prof. Luigi Sofo, Prof. Antonio Tortorelli pamoja na Prof. Roberta Menghi. 

Wengine katika jopo hili la madaktari ni Prof. Massimo Antonelli, Prof. Liliana Sollazzi pamoja na Madaktari Roberto De Cicco na Maurizio Soave. Kwenye chumba cha upasuaji, walikuwepo pia Prof. Giovanni Battista Doglietto pamoja na Prof. Roberto Bernabei.

Taarifa ya madaktari wa Hospitali ya Gemelli inaonesha kwamba, operesheni hii imefanikiwa na Baba Mtakatifu Francisko anaendelea vyema. Kama kawaida yake katika hali ya unyenyekevu, Baba Mtakatifu Francisko, baada ya sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 majira ya jioni alipelekwa Hospitalini Gemelli kama wagonjwa wengine na kulazwa ghorofa ya 10 katika chumba ambazo kwa muda mrefu Mtakatifu Yohane Paulo II alikitumia wakati wa matibabu hospitalini hapo. 

Prof. Sergio Alfieri, mwenye umri wa miaka 55 ndiye daktari mkuu wa kitengo cha magonjwa ya mfumo wa chakula.

Takwimu zinaonesha kwamba, kama daktari amekwisha kufanya operesheni za magonjwa ya mfumo wa chakula zipatazo 9, 000 tangu mwaka 2010. 

Prof. Sergio Alfieri ni kati ya wanafunzi waliofundwa na kufundika kutoka katika Jopo la Madaktari bingwa Francesco Crucitti, ambaye katika historia anatambulikana kama Daktari aliyemfanyia Mtakatifu Yohane Paulo II, operesheni tatu. Alifundwa pia na Profesa Giovanni Battista Doglietto. 

Radio Vatican itaendelea kukujuza yale yanayojiri katika afya ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anapumzika Hospitalini Gemelli baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa kwenye utumbo mpana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news