RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 27, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) Dkt. John Nkengasong Ikulu jijini Dar es Salaam.
Dkt. Nkengasong amempongeza Rais Samia kwa hatua mbalimbali anazochukua katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 na kusema kuwa Africa CDC kinaunga mkono jitihada hizo za Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Amesema Africa CDC, imedhamiria kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ikiwemo Tanzania kuweka mipango ya pamoja na kutumia fursa zinazopatikana kupitia kituo hicho katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa chanjo na usambazaji wake.
Aidha, Dkt. Nkengasong amesema Africa CDC wameanzisha mpango wa Safari za Kuaminika (Trusted Travel) utakaowawezesha wanachama wa AU kusafiri ndani na nje ya Bara la Afrika bila vikwazo vitokanavyo na ugonjwa wa UVIKO 19.
Dkt. Nkengasong ametaja maeneo mengine ambayo Africa CDC inaweza kushirikiana na Tanzania kuwa ni kuzijengea uwezo maabara na wataalamu ili kuimarisha upimaji na utambuzi wa aina mbalimbali za virusi (variant) vya UVIKO 19, pamoja na kusaidia masuala ya utafiti , kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na UVIKO 19 na kupokea chanjo.
Ameongeza kuwa Africa CDC kupitia Jukwaa la UVIKO 19 litaziwezesha nchi za Afrika kununua bidhaa za kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 kwa pamoja. Kupitia kikosi kazi maaalum, Africa CDC inakusudia kufanya manunuzi ya pamoja ya chanjo zote zinazohitajika katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.
Kwa upande wake Rais Samia amemshukuru Dkt. Nkengasong kwa uamuzi wake wa kuja Tanzania kwa lengo la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali na kumjulisha kuwa tayari Tanzania ina Kamati Maalum ya kitaifa inayoratibu masuala yote yanayohusu ugonjwa wa UVIKO 19 na ipo tayari kufanya kazi na wataalamu kutoka Africa CDC katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Mhe. Rais Samia amesema mbali na kamati hiyo, Serikali imeboresha huduma za Afya kwa kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19.
Katika mazungumzo hayo Rais Samia amesema Tanzania imejiunga na Mpango wa Covax (Covax facility) kwa lengo la kunufaika na fursa zitokanazo na mpango huo ikiwemo upatikanaji wa chanjo.
Aidha, Mhe. Rais amesema kupitia Mpango wa Tatu wa Taifa wa miaka mitano wa Maendeleo (FYDP III), Serikali inakusudia kujenga viwanda vya kuzalisha chanjo za aina mbalimbali katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Amesema Africa CDC ni muhimu katika kusaidia kutoa elimu kwa wanadiplomasia wetu ili kufahamu masuala ya afya na kuweza kushiriki kikamilifu katika mikutano inayohusu masuala hayo katika maeneo yao.
Mhe. Rais Samia amemhakikishia Dkt. Nkengasong kuwa Tanzania iko tayari kufanya kazi na Africa CDC haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na ongezeko la kusambaa kwa ugonjwa wa UVIKO 19 katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.