RC PWANI APOKEA CHANJO 6000 ZA UVIKO -19,AZINDUA RASMI ZOEZI LA CHANJO HIZO

Na Rotary Haule,Kibaha

MKOA wa Pwani umepokea chanjo aina ya Johnson Johnson dozi elfu sita (6000) kwa ajili ya kinga kwa wananchi wake dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.

Chanjo hiyo imepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge na kwenda sambamba na uzinduzi wa utoaji wa chanjo hiyo uliofanyika katika eneo la Kituo cha afya Mkoani kilichopo Mjini Kibaha.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,akichanjwa chanjo ya Uviko-19 ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa chanjo hiyo kwa wananchi wake uliofanyika katika kituo cha afya Mkoani kilichopo Mjini Kibaha.(Picha na Rotary Haule).

Akizungumza katika uzinduzi huo Kunenge alisema kuwa chanjo hiyo ni salama na itatolewa kwa hiari kulingana na mahitaji ya mtu husika.

Kunenge,alisema kuwa anamshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu na upendo mkubwa kwa wananchi wake juu ya chanjo hiyo.

Alisema kuwa,pamoja na kuwepo kwa chanjo hiyo lakini ni lazima wananchi waendelee kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya.

Alisema ,moja ya maelekezo hayo ni kunawa mikono kwa maji tiririka,kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono (Sanitizer) pamoja na kuzingatia umbali wa mtu na mtu (Social distance).

"Msimamo wa Serikali ni kuwa chanjo hiyo ni hiari na hakuna mtu wa kulazimishwa na sisi Pwani tumepata kiasi ambayo tunaweza kuanza nayo kwa kuchanja makundi maalum na makundi mengine yatafuata kulingana na mahitaji,"alisema Kunenge.

Aidha, Kunenge aliongeza kuwa mkoa wa Pwani unachangamoto ya wagonjwa wa Uviko-19 ingawa haulingana na Mikoa mingine lakini kikubwa ni kuhakikisha kila mwananchi analinda afya yake.

Kwa upande wake mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani, Gunini Kamba alisema kuwa, chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote.

Kamba alisema, kwa hatua ya awali chanjo hiyo itayalenga makundi maalum yanayotoa huduma kwa jamii kama vile watumishi wa Serikali,watu wenye umri zaidi ya miaka 45,walimu,wanajeshi,wasafiri wa kimataifa, wageni kutoka nje,watu wa viwanda na wataalamu mbalimbali.

Hatahivyo,Kamba alisema chanjo hiyo itatolewa katika vituo maalum vilivyoainishwa katika kila Wilaya na kila mwananchi mwenye kuhitaji atapata kulingana na maeneo aliyopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news