Serikali yawaita Watumishi 473 walioomba kazi Sekta ya Afya

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

SERIKALI imetangaza kuwaita kazini watumishi wa afya 473 walioomba nafasi za kazi kwenye kada mbalimbali za Wizara ya Afya.
Akizungumza leo Julai 5,2021  jijini hapa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Professa Abel Makubi amesema, nafasi hizo za ajira na mgawanyo wa kada mbalimbali zinatokana na Watumishi kukoma utumishi wao kwa sababu mbalimbali kama vile kuacha kazi,kufariki na kustaafu.

Professa Makubi amesema, nafasi hizo 473 zilitangazwa kwenye tovuti ya Wizara ya Afya Mei 12, mwaka huu na kufunga Mei 25, 2021 mwaka huu.

"Jumla ya maombi yaliyopokelewa kwenye mfumo yalikuwa 19,757 na kati ya hayo waombaji 4,760 hakukamilisha ujazaji wa fomu hadi hatua ya mwisho hivyo maombi yaliyofanyiwa uchambuzi ni 14,997,"amesema.

Ameongeza kuwa, "baada ya uchambuzi kufanyika jumla ya maombi 9,338 yalikidhi vigezo vya kuajiriwa kutokana na tangazo letu,"amesema Profesa Makubi.

Aidha,  amesema katika kuwapata waombaji wa kujaza nafasi zinazohitajika vigezo vya ziada vilitumika anbavyo waombaji wenye ulemavu walipewa kipaumbele,waliohitimu elimu mwaka 2018 na kurudi nyuma wenye ajira za mkataba wa muda na wenye umri chini ya miaka 45.

Sambamba na hayo amesema baada ya uchambuzi zaidi kufanyika jumla ya waombaji 473 waliohitajika wamechaguliwa na wamepangwa kwenye maeneo ya uhitaji na upungufu mkubwa wa Watumishi.

PROFESSA MAKUBI AELEZA SABABU ZA WALIOKOSA SIFA


Amesema ni pamoja na kushindwa kukamilisha ujazaji wa fomu mpaka hatua ya mwisho,kukosa sifa za kimuundo za kada husika,kutoambatanisha vyeti muhimu wakati wa kuomba ajira, kutokuwa na leseni za kitaaluma pamoja na leseni kuisha muda wake na baadhi ya waombaji kuomba kazi katika kada ambayo siyo ya taaluma yao.

"Naomba nitumie fursa hii kuwasihi waombaji wa kazi za ajira zinazotangazwa kuwa makini wakati wanapowasilisha maombi ya kazi,"amesema.

Ameongeza kusema kuwa, "waombaji wanaosimamiwa na mabaraza mbalimbali ya kitaaluma wahakikishe wanakuwa na leseni hai za kufanya kazi,"amesema.

Ameeleza kuwa, waombaji wote waliofaulu na ambao majina yao yameorodheshwa kwenye matangazo wanatakiwa waripoti kwenye Ofisi za Wizara ya Afya zilizopo katika ukumbi wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Mirembe kuanzia tarehe 5 hadi 9 Julai, mwaka huu.

Hata hivyo, amewataka waombaji waambatanishe vyeti halisi vya elimu na taaluma yake aliyotumia kuomba ajira ikiwa ni pamoja na nakala mbili ya cheti cha kuzaliwa,wasifu binafsi (CV),Nakala ya jitambulishe, namba ya uraia (NIDA), picha 2 za passport size ,Nakala ya Elimu ya Sekondari na kidato cha sita,Nakala ya vyeti vya taaluma,Nakala ya Cheti Cha mafunzo na nakala ya Cheti Cha usajili kutoka Baraza husika.

Pia kuambatanisha nakala za ithibati ya vyeti vya elimu na taaluma fc kutoka TCU na Necta kwa wale waliosoma vyuo vya nje pamoja na wale waliosoma sekondari nje ya nchi au mitaala ya nje.

"Endapo majina yako yanatofautiana kwenye vyeti vyako pamoja na cheti cha kuzaliwa hakikisha unawasilisha kiapo cha majina kutoka kwa msajili wa viapo na kusajiliwa na msajili wa hati,Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi"amesema Makubi.

Amesema, mtumishi atakayeripoti na nakala pungufu ya vielelezo tajwa hapo juu hatopokelewa na pia waombaji wote ambao majina yao hayataonekana katika tangazo wafahamu kuwa hawakupata nafasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news