Spika Ndugai agongea msumari tozo za miamala ya simu

Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesisitiza kuwa suala la tozo za miamala lilipitishwa na kutungiwa sheria bungeni, hivyo ni lazima litekelezwe kwa maslahi ya taifa na jamii kwa ujumla.

Aidha, amewataka wananchi wanaolalamika kuja na njia mbadala ya namna serikali itakavyoweza kupata fedha ili kufanikisha miradi ya kimaendeleo.
Ndugai ametoa kauli hiyo leo jijini hapa katika kikao cha watendaji wa mkoa wa Dodoma na wilaya kujitathimini katika utekelezaji wa majukumu yao, kwani serikali imekuwa ikitimiza wajibu wake kwa kuleta fedha kwa wakati, lakini tatizo lipo kwa watendaji.

Amesema, wabunge waliamua kupitisha suala hilo la miamala na tozo kwa kuwa fedha inayopatikana katika eneo hilo ni nyingi na inaweza kuisaidia serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Spika amesema kuwa, fedha itakayopatikana inakwenda katika mfuko maalum, na zinakwenda kuwasaidia wananchi kupata huduma muhimu zikiwemo umeme, maji, kujenga madarasa, madaraja, kupitia tozo hizo walizozipitisha.

"Ndio mana sisi wabunge tukaamua kwenda kwenye suala la miamala kwa sababu tunauhakika fedha itakayopatikana itasaidia katika miradi ya maendeleo.

"Tumepitisha sisi tukatunga sheria sisi, tunataka kuliona hilo, hakuna njia ya mkato sasa wewe ambaye unapinga tupe njia mbadala tutapata wapi fedha, tunafikaje 2025, kwa hiyo maamuzi ni hayo tumeyafanya, kwa nia njema kabisa kwamba 2025 tuwe tumetoka, tuwe ni taifa la Tanzania ambalo ni tofauti Tanzania nzima, CCM oyeeee,"amesema Ndugai.

Amesema, wanataka watu na watoto wao waweze kupata huduma zote muhimu zikiwemo za madarasa mazuri, huduma za bora za afya na nzuri kama wananchi waishio maeneo ya vijijini.

Akizungumzia kuhusu mkoa wa Dodoma amewataka watendaji wa mkoa wa Dodoma kujitathimini katika utekelezaji wa majukumu yao, kwani serikali imekuwa ikitimiza wajibu wake kwa kuleta fedha kwa wakati lakini tatizo lipo kwa watendaji.

"Hapa nitolee mfano mkuu wa mkoa wa Antony Mtaka aliyetoka Simuyu kule alifanya kazi nzuri, hivyo hapa akishindwa kufanya vizuri tujue kabisa tatizo lipo kwetu,"amesisitiza Ndugai.
Awali akifungua kikao kazi hicho, Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amebainisha vipaumbele vinne ambavyo atavisimamia katika mkoa wa Dodoma.

"Vipaumbele nitakavyovisimamia katika uongozi wangu ni pamoja na Elimu, migogoro ya Ardhi, kilimo na ufugaji wenye tija na huduma bora za sekta za afya,"amesema huku akitangaza alizeti kuwa zao la biashara katika mkoa huo.

Kuhusu lengo la kikao hicho mkuu huyo wa mkoa amesema lengo la kikao hicho ni kwenda pamoja kama timu katika kutekeleza mambo yanayohusu maendeleo.

"Nawasii tuwe na lugha ya pamoja yapo mambo mazuri wenzetu wameyafanya hivyo lazima tuyaendeleze, sisi Dodoma tuna utofauti tunabeba haiba ya makao makuu ya nchi hivyo ni lazima tuwe na matarajio makubwa,"amesema.

Akizungumzia kiwango cha elimu amesema mkoa wa Dodoma upo katika hali mbaya, katika ngazi zote ikiwemo mitihani ya moku, mkoa haujafanya vizuri hivyo zinahitajika jitihada za ziada kuhakikisha mkoa unafanya vizuri katika sekta ya elimu na kuondokana na aibu iliyopo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema Halmashauri zote nane za mkoa wa Dodoma kuwa na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitauingizia mkoa fedha za kutosha kuendesha miradi mbalimbali.

Ameeleza jiji la Dodoma lilikusanya sh.bilioni 70 kutokana na mauzo ya viwanja sasa wapo kiwango cha sh.bilioni 30 hivyo lazima watafute vyanzo vipya vya mapato na anatamani kuona ubunifu katika suala hilo.

Pia ameeleza kuwa anatamani kuona kaya zikipanda miti mingi kwa ajili ya utunzaji wa mazingira pamoja na kuweka mipango mizuri ya utunzaji wa mazingira katoka mkoa.

Pia Mtaka amewaonya watumishi wa mkoa wa Dodoma kuacha tabia ya uongo , kufitiniana na kuchonganishana maana ni tabia ambayo inamchukiza sana

"Watumishi waongo na wachonganishi hawana nafasi kwangu, watu wanachonganisha watu ni wabaya , tumekutanishwa na kazi tufanye kazi tuheshimiane kiongozi haongozwi,"amesisitiza Mtaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news