Na Mathew Kwembe, Arusha
Mabingwa wa Netiboli wa Ligi ya Muungano wa mwaka 2019, timu ya TAMISEMI Queens kutoka Dodoma haishikiki katika michuano inayoendelea ya ligi daraja la kwanza inayoendelea katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha baada ya leo kuisambaratisha timu ya Polisi ya Arusha kwa magoli 62-24.
Katika pambano hilo kali na la kusisimua hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika timu ya TAMISEMI QUEENS ilikuwa ikiongoza kwa magoli 14-5, robo ya pili iliongoza kwa magoli 27-12, na robo ya tatu ubao ulisomeka timu hiyo ikiongoza kwa magoli 48-17.
Mchezaji Aziza Itonye (GA) kutoka TAMISEMI QUEENS akijaribu kufunga mojawapo ya magoli huku akichungwa na golikipa wa Polisi Arusha Eva Jimmy ambapo TAMISEMI ilishinda 62-24.
Nyota wa mchezo wa leo alikuwa ni mchezaji wa kati wa TAMISEMI QUEENS Sophia Komba (C), ambaye mara kwa mara alikuwa akigawa mipira ya hatari kwenye goli la polisi Arusha na kama siyo uhodari wa wachezaji wa maafande hao chini ya Julieth Martin (GD) na Eva Jimmy (GK) TAMISEMI QUEENS ingekuwa na kalamu ya magoli.
Magoli ya TAMISEMI QUEENS yalifungwa na Lilian Jovin (GS) na Aziza Itonye (GA) huku magoli ya polisi Arusha yakifungwa na wachezaji Diana Dickson (GS) na Jenipha Saning’o (GA).
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, nahodha msaidizi wa TAMISEMI QUEENS Sophia Komba alisema kuwa mchezo ulikuwa mzuri kwani timu yake imejiandaa vya kutosha ili kulibeba kombe hilo.
Mshambuliaji wa pembeni wa polisi Arusha Khadija Ramadhani (WA) akichungwa kwa makini na Semeni Abeid (WD) wa TAMISEMI QUEENS ili asilete madhara huku wachezaji Aziza Itonye, Mersiana Kizenga na golikipa Chuki kikalao (kulia) wakifuatilia kwa makini mpira huo.
Naye Kocha wa TAMISEMI QUEENS Maimuna Kitete amesema timu yake imekuja kupambana na haiiogopi timu yeyote katika mashindano hayo kwani kwao kila mechi ni fainali na kwamba vijana wake wapo vizuri kwa michezo ijayo.
Matokeo ya michezo mingine iliyochezwa jana na leo inaonyesha Magereza Morogoro imeifunga Uhamiaji magoli 39-38, JKT Mbweni imeifunga Polisi Arusha 66-23, Smart imeifunga Muungano magoli 38-26, Mgulani JKT imeichapa Ihumwa Dream Team magoli 40-26 na JKT Mbweni imeifunga Jiji Arusha 97-21.
Benchi la ufundi la TAMISEMI QUEENS likiongozwa na Kocha Maimuna Kitete (kulia) waliokaa na msaidizi wake Neema Chongolo wa nne kutoka kulia wakifuatilia kwa makini mchezo baina ya timu yao dhidi ya Polisi Arusha ambapo TAMISEMI ilishinda magoli 62-24
Ligi hiyo itaendelea tena hapo kesho kwa mchezo kati ya TAMISEMI QUEENS dhidi ya Ihumwa Dream Team, Polisi Arusha dhidi Eagle Queens na Magereza Morogoro dhidi ya NVRF QUEENS
Jumla ya timu 12 za wanawake na timu 4 za wanaume zinashiriki kwenye ligi hiyo.
Tags
Michezo