TAMISEMI QUEENS NA MBWENI JKT ZAWA TISHIO LIGI DARAJA LA KWANZA NETIBOLI

Na Mathew Kwembe, Arusha

Timu za Mbweni JKT ya jijini Dar es salaam na TAMISEMI QUEENS kutoka jijini Dodoma zimegeuka kuwa mwiba mkali kwa timu nyingine zinazoshiriki mashindano ya Netiboli ligi daraja la kwanza yanayoendelea katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ya jijini Arusha baada ya kufanikiwa kuzifunga timu zote ilizokutana nazo.
Wachezaji wa timu ya Mbweni JKT (Jezi nyekundu) wakichuana vikali na wachezaji wa timu ya Ihumwa Dream Team (Jezi ya blue) katika mchezo uliochezwa leo ambapo Mbweni ilishinda kwa magoli 78-30. 
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Netiboli Tanzania (CHANETA) Judith Ilunda hadi kufikia jana bingwa mtetezi timu ya JKT Mbweni ndiyo ilikuwa ikiongoza ligi hiyo baada ya kucheza michezo 5 na kushinda michezo yote, na kujikusanyia alama 10, na kufuatiwa na TAMISEMI QUEENS ambayo ilijikusanyia alama 8 baada ya kucheza michezo 4.

Magereza Morogoro inashika nafasi ya 3 kwa kuwa na alama 8 baada ya kucheza michezo 6, huku nafasi ya 4 na ya 5 zikichukuliwa na timu za majeshi za Uhamiaji na Mgulani JKT ambapo Uhamiaji ina alama 6 baada ya kucheza michezo 5 huku Mgulani JKT ikishika nafasi ya 5 baada ya kucheza michezo 5.

Nafasi ya 6 imeshikwa na timu ya Polisi ya Arusha yenye alama 3 baada ya kucheza michezo 6, huku nafasi ya 7, 8 na 9 zikichukuliwa na Ihumwa Dream Team, Eagles na Jiji Arusha.
Wachezaji wa JKT Mgulani (Jezi rangi ya chungwa) wakitafuta mbinu za kuwatoka wachezaji wa TAMISEMI QUEENS (Jezi rangi ya kijani) wakati timu hizo zilipochuana leo asubuhi ambapo TAMISEMI ilishinda kwa magoli 46-32. 

Ligi hiyo iliendelea tena leo ambapo asubuhi JKT Mbweni ilicheza na Ihumwa Dream Team na matokeo JKT Mbweni ilishinda kwa magoli 78-30, nayo timu ya TAMISEMI QUEENS ilicheza michezo miwili na kufanikiwa kushinda michezo yote.

Katika mchezo wa kwanza, TAMISEMI QUEENS ilicheza dhidi ya JKT Mgulani na kuifunga magoli 46-32 na katika mchezo wa pili TAMISEMI QUEENS ilicheza dhidi ya Uhamiaji na kuifunga magoli 49-32.

Kwa matokeo hayo TAMISEMI QUEENS na JKT Mbweni zote zimecheza michezo 6 kila mmoja, na kufanikiwa kushinda michezo yote, hali inayoashiria upinzani mkali katika kinyang’anyiro cha kumtafuta bingwa wa ligi daraja la kwanza netiboli nchini mwaka huu.
Wachezaji wa timu ya TAMISEMI QUEENS wakiwa na viongozi wao kabla ya mchezo wao na JKT Mgulani eo asubuhi ambapo TAMISEMI ilishinda kwa magoli 46-32. 
Mchezaji wa kati wa TAMISEMI QUEENS Sophia Komba akitafuta mbinu za kuwatoka walinzi wa uhamiaji huku mshambuliaji wa pembeni wa TAMISEMI QUEENS Lilian Jovin akiwa tayari kutoa msaada katika mchezo uliochezwa leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jini Arusha ambapo TAMISEMI QUEENS ilishinda kwa magoli 49-32.

Timu hizo mbili zinatarajiwa kukutana katika mchezo wa mwisho wa kuhitimisha mashindano ya ligi daraja la kwanza utakaofanyika tarehe 29 julai, 2021, mchezo ambao huenda ndiyo utakaoamua hatma ya ubingwa wa netiboli ligi daraja la kwanza mwaka huu

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news