TAMISEMI QUEENS YAANZA KWA KISHINDO LIGI DARAJA LA KWANZA

Na Mathew Kwembe, Arusha

Michuano ya Netiboli ligi daraja la kwanza ambayo imeanza jana katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid hapa jijini Arusha imeshuhudia timu ya netiboli kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ‘TAMISEMI QUEENS’ ikiyaanza mashindano haya kwa kishindo kwa kuikung’uta bila huruma wenyeji wa mashindano haya Jiji Arusha magoli 92-15.

Magoli ya TAMISEMI QUEENS yalifungwa na wachezaji Lilian Jovin, Aziza Itonye na Dorice Antony.
Wachezaji wa TAMISEMI QUEENS na Jiji Arusha wakiwania mpira katika mojawapo ya purukushani za mchezo wa jana wa Netiboli ligi daraja la kwanza ambapo TAMISEMI QUEENS waishinda magoli 92-15.

Katika mcheo huo mkali na wa kusisimua timu hiyo ya ‘TAMISEMI QUEENS’ imeonyesha dhamira yake ya kulitwaa kombe hilo kufuatia wachezaji wake hatari wakiongozwa na Lilian Jovin kuzifikia nyavu za Arusha Jiji mara kwa mara.

Kocha wa ‘TAMISEMI QUEENS’ Maimuna Kitete amesema kipigo walichokipata Arusha Jiji ni salamu tosha kwa timu nyingine zinazoshiriki michuano hiyo kuwa timu yake ina dhamira ya kulibeba kombe hilo.

Mwaka 2019 wakati mashindano hayo yalipofanyika katikwa uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ‘TAMISEMI QUEENS’ ilishika nafasi ya nne, na kushiriki ligi ya netiboli ya muungano mjini Zanzibar ambapo ililitwaa kombe la Muungano.
Wachezaji wa TAMISEMI QUEENS wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo baina yao na Jiji Arusha.

TAMISEMI Queens ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Muungano kwa kuisambaratisha timu ya Mbweni JKT kwa jumla ya magoli 40 kwa 32 katika mchezo wa fainali uliopigwa katika viwanja vya Gymkana Kisiwani Zanzibar.

Katika michezo mingine ya ligi daraja la kwanza iliyochezwa jana timu ya Magereza Morogoro iliifunga Ihumwa Dream Team ya Dodoma magoli 54-30, na JKT Mgulani iliichalaza Eagle Queens magoli 43-26.
Kocha wa TAMISEMI QUEENS Maimuna Kitete kushoto na Meneja wa timu hiyo Doto Bintaraba wakifuatilia kwa makini mchezo kati ya TAMISEMI QUEENS dhidi ya Jiji Arusha ambapo TAMISEMI QUEENS walishinda mchezo huo kwa magoli 92-15.

Mapema leo asubuhi kutakuwa na sherehe za ufunguzi rasmi wa michuano hiyo ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Judith Ilunda.

Michuano hiyo itaendelea tena jioni kwa michezo kati ya Mgulani JKT itakayocheza na NVRF Queens, JKT Mbweni wataonyeshana kazi na Jiji Arusha huku Magereza Morogoro wakipangiwa kucheza na Uhamiaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news